Ronaldo na Al Nassr wameanza msimu wao wa Asian Champions League kwa kuifunga Persepolis ya Iran / Picha: Reuters

Klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia imeanza msimu wake wa ligi ya mabingwa bara Asia AFC kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Persepolis FC ya Iran katika mechi ya Kundi E iliyopigwa Uwanja wa Azadi.

Cristiano Ronaldo alifungua ukurasa wake mpya kwenye ligi ya mabingwa bara Asia AFC na klabu yake ya Al Nassr kwa kuiongoza timu hiyo kujipatia ushindi wake ugenini.

Persepolis FC walilazimika kucheza na wachezaji kumi pindi kiungo wa Iran Milad Sarlak alipolishwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi yake ya pili ya njano katika kipindi cha pili kwa kumkanyaga Ronaldo.

Nahodha wa Ureno, Ronaldo alichangia bao la kwanza la Al Nassr kwa kubadilishana pasi moja-mbili na Brozovic ndani ya sanduku la timu ya Persepolis na kumuandalia Abdulrahman Ghareeb aliyefanikiwa kuipa Al Nassr goli muhimu la ufunguzi na la ugenini katika dakika ya 62.

Ronaldo na timu yake ya Al Nassr sasa watacheza mechi yao ijayo nyumbani ambapo wataikaribisha mabingwa wa ligi ya Tajikistan Isiklol katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha King Saud mjini Riyadh.

Hata hivyo, mechi hiyo ilichezwa bila mashabiki kutokana na marufuku iliyowekwa na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) kwa klabu ya Persepolis kama adhabu kwa kuweka chapisho lenye utata kwenye mitandao yao ya kijamii kuhusu taifa la India.

TRT Afrika