Michael Olunga ameteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora Mashariki ya kati 2023. Picha: Getty

Nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars, Michael Olunga, anayechezea klabu ya Qatar ya Al Duhail ameteuliwa kugombea tuzo ya mwanasoka bora Mashariki ya Kati dhidi ya nyota mbali mbali akiwemo Cristiano Ronaldo anayechezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia kwenye tuzo za Dubai Globe Soccer zitakazofanyika Januari 19 2024.

Olunga ni mmoja wa wachezaji 12 walioteuliwa kuwania katika kipengele hicho kilichowajumuisha Ronaldo, Benzema, Salem Al-Dawsari, Mourad Batna, Mohamed El Shenawy, Abderrazak Hamdallah, Odion Ighalo, Ali Mabkhout, Riyad Mahrez, Alejandro Romero na Talisca.

Uteuzi huu unajiri siku chache tu baada ya Olunga kufunga magoli mawili na kuipa Kenya ushindi wa 5-0 dhidi ya Ushelisheli mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Msimu huu unaoendelea wa 2023-2024, Olunga tayari ameifungia Al Duhail magoli 7.

Msimu uliopita wa 2022-2023, Olunga alifanikiwa kufunga magoli 22 na msimu wa 2021-2022, Olunga aliifungia Al Duhail SC magoli 24, na kumaliza mfungaji bora misimu miwili mfululizo.

Aidha, mnamo mwaka wa 2021, Olunga wa klabu ya Qatar Al Duhail alitawazwa kuwa mfungaji bora wa ligi ya mabingwa bara Asia 2021 kwa kufunga mabao 9.

Licha ya uteuzi huu, Olunga na wachezaji wenza wa Al Duhail wameendelea na mazoezi yao wakijiandaa kuchuana na Al Istiklol Dushanbe kutoka Tajikistan.

Al Duhail itakuwa nyumbani uwanjani Abdullah bin Khalifa kupiga mechi ya raundi ya 5 ya ligi ya mabingwa bara asia AFC dhidi ya Al Istiklol Dushanbe.

Aidha, klabu ya Olunga ya Al Duhail imefuzu kucheza robo fainali Kombe la Ooredoo baada ya kumaliza wa pili nyuma ya Al Rayyan katika kundi B, ikiwa na pointi 9.

TRT Afrika