Real Madrid wako kwenye nusu fainali nyingine baada ya kuifunga Chelsea 2-0 kwa ushindi wa jumla wa 4-0 kwenye robo fainali.
Rodrygo alifunga mabao mawili dakika ya 58 na 80 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge Mjini London.
Real Madrid imefuzu kwa nusu fainali ya Champions League mara 11 katika misimu 13 iliyopita.
Kwa upande mwengine, AC Milan ilifuzu kuingia nusu fainali ya UEFA Champions League baada ya ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Napoli Jumanne.
Dakika ya 21, AC Milan walipata penalti baada ya Mario Rui kumuangusha Rafael Leao kwenye Uwanja wa Stadio Diego Armando Maradona.
Lakini penalti ya Olivier Giroud iliokolewa na kipa Alex Meret.
AC Milan walitinga wavuni kwa kumalizia kwa shuti la karibu la Giroud katika shambulizi la haraka huku Leao akiwapiga chenga walinzi wa wapinzani wao na kufanya pasi nzuri dakika ya 43.
Dakika ya 82, Napoli walipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha mechi dhidi ya AC Milan huku fowadi wa Georgia Khvicha Kvaratskhelia akikosa penalti muhimu nyumbani.
Napoli walipata bao la dakika za lala salama la Victor Osimhen, lakini halikutosha kushinda kwa hatua inayofuata hivyo mkondo wa pili wa robo fainali ulimalizika kwa matokeo ya 1-1 huko Napoli.
Ratiba ya Jumatano kwa mechi za robo fainali ya mkondo wa 2: Bayern Munich - Manchester City (0-3) Inter Milan - Benfica (2-0)