Ni kitu gani kinafanya mashindano ya Kombe la Dunia Qatar kuwa ya kipekee?

Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kung’oa nanga kwa mashindano ya Kombe la dunia nchini Qatar, tayari upekee wa mashindano hayo ni wazi ikizingatiwa kuwa yatafanyika kipindi cha majira ya baridi katika ulimwengu wa kaskazini. Mashindano hayo yatang’oa nanga tarehe Novemba 20 na kufululiza mpaka tarehe 18 Disemba.

Kawaida mashindano haya hufanyika majira ya joto lakini kutokana na kiwango cha juu cha joto ambacho hushuhudiwa Qatar, ikabidi yafanyike mwishoni mwa mwaka huu. Hii ina maana ligi kuu za bara ulaya zitachukua likizo ili kupisha mashindano hayo.

Itakuwa pia ni mara ya kwanza kwa nchi ya Uarabuni kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia.

Aidha itakuwa ni mara ya kwanza kwa bara Asia kuwa mwenyeji wa mashindano hayo tangu mwaka 2002 ambapo Korea Kusini na Japan zilikuwa mwenyeji na taifa la Brazil likatwaa taji la mashindano hayo.

Nchi ya Brazil imeshinda taji hilo mara tano na mwaka huu nyota wao kama vile Neymar Junior wanatarajiwa kutikisa Qatar. Brazil walishinda taji hilo mara ya mwisho mwaka 2002 walipowanyuka Ujerumani magoli mawili kwa nunge huko Yokohama, Japan.

Wengine wanaotarajiwa kuonesha ushindani mkali ni Ufaransa wakiwa na nyota kama vile Kylian Mbappe, Paul Pogba na Antoine Griezmann. Ikumbukwe Ufaransa ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia.

Ujerumani pia inatarajiwa kuonesha ushindani mkali nchini Qatar ikiwa inajivunia ushindi wa kombe hilo mara nne.

Italia haitakuwepo katika mashindano hayo kwani haikufuzu kushiriki lakini imeshinda kombe hilo mara nne(1934, 1938, 1982 na 2006).

Taifa la Qatar litashiriki kwa mara ya kwanza huku Wales na Canada wakirejea baada ya kipindi kirefu. Qatar ipo kwenye Kundi A pamoja na Ecuador, Senegal na Uholanzi.

Wales wapo kwenye kundi B pamoja na Uingereza, Iran na Marekani.

Kwenye kundi F Canada nayo itagaragazana na Ubelgiji, Morocco na Croatia. Ikumbukwe Ubelgiji ilimaliza ya tatu mwaka 2018 nchini Urusi huku Croatia ikimaliza ya pili.

TRT World