Mukhtar Ali, staa mwenye asili ya Kisomali anayecheza na Ronaldo AL Nassr, nchini Saudia

Mukhtar Ali, staa mwenye asili ya Kisomali anayecheza na Ronaldo AL Nassr, nchini Saudia

Cristiano Ronaldo aliisaidia Al-Nassr kuilaza Al-Hilal na kutwaa taji lao la kwanza la Kombe la Klabu Bingwa ya Kiarabu
Mukhtar Ali, ni raia wa Saudi Arabia mwenya Asili ya Somalia. Picha: Al Nassr

Klabu ya Al Nassr, ilipokuwa ikifurahia ubingwa wake, miongoni mwa nyota wake waliopokezwa medali ya dhahabu kwa kutwaa ubingwa, ni Mukhtar Ali, kiungo mwenye asili ya Somalia, aliyepewa uraia wa Saudi na kuitwa timu ya taifa.

Mukhtar alisajiliwa na Al Nassr mnamo Agosti 2019 kutoka Vitesse ya Uholanzi huku kiungo huyo akisaini mkataba wa hadi 2025 kuichezea klabu hiyo.

Mukhtar Alia sherekea ushindi wa Saudi Arabia. Picha: Mukhtar Ali 

Ingawa wazazi wake walizaliwa Somalia, Mukhtar Ali alizaliwa mjini Jeddah, nchini Saudia na hata kuchagua kuichezea timu ya taifa ya soka ya Saudi Arabia. Mukhtar alikuwa kwenye kikosi cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 waliotinga fainali ya mashindano ya bara Asia mnamo Januari 2020 ingawa Saudia ilifungwa na Korea Kusini kwenye fainali.

"Saudi Arabia ilitamani niiwakilishe, walitaka nicheze na sio kama hatukujua chochote kuhusu Saudi Arabia. Wazazi wangu walikulia Saudi Arabia. Kwa hivyo, shirikisho lilipowasiliana, niliamua kwenda kuangalia jinsi lilivyo, kiwango na kila kitu. Kiwango ni kizuri sana. Watu, mpira wa miguu, kwa hivyo sikuweza kusema hapana." Alisema Mukhtar.

Licha ya tovuti rasmi za Chelsea, Vitesse, majarida mbalimbali, na blogu kusema kuwa Mukhtar alizaliwa Mogadishu, nyota huyo mwenye umri 25, mwenyewe anasema alizaliwa Jeddah.

Ni heshima kubwa kwa taifa la Somalia na familia yangu kwamba mwanangu Mukhtar, ambaye ni maarufu na katika soka ya ngazi ya juu, amefikia kiwango cha kimataifa, na ufanisi wa Mukhtar sasa ni msukumo kwa vijana wengine wanaopenda taaluma hii.

Ali Abdullahi ambaye ni babake mchezaji wa Saudi Arabia na Al Nassr Mukhtar Ali.

Kiungo huyo wa kati, ambaye anasema ametembelea Somalia mara moja tu, alifuatiliwa kwa karibu na kocha wa zamani wa Saudi Arabia Edgardo Bauza na kualikwa kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Saudia kwenye kambi maalum kwa wachezaji wanaojulikana kama, "muwallid," neno linalotolewa kwa watu waliozaliwa katika Ufalme huo kwa wazazi wa kigeni.

Ali Abdullahi Sheikh (Ali Afgooye) ambaye ni baba wa mchezaji huyo wa Saudi Arabia Mukhtar Ali, alikua nchini Saudia na kuhamia London na familia nzima Mukhtar alipokuwa mchanga na hivyo basi kupelekea nyota huyo kuiwakilisha uingereza katika vitengo vya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 16 na umri wa miaka 17.

Mukhtar Ali, jezi nambari (11) akiwa kwenye timu ya taifa ya Saudi Arabia. Picha: Shirikisho la Soka Saudia. 

Mukhtar Ali, alikuwa miongoni mwa nyota chipukizi wa timu ya vijana wa Chelsea waliofanikiwa kwa kushinda Kombe la Vijana la FA misimu mitatu mfululizo, na vile vile Kombe la Vijana la FA na Ligi ya Vijana ya UEFA wakati waliponyakua vikombe mara mbili mnamo 2016.

Al-Nassr iliishinda Al-Hilal na kutwaa taji lao la kwanza la Kombe la Klabu Bingwa ya Kiarabu. Picha: Al Nassr

"Watu wengi wanafikiria kuwa nilihamia Saudi Arabia kwa ajili ya pesa, lakini hiyo haikuwa sababu. Niliangalia chaguzi zangu na kufikiria juu ya taaluma yangu ya kimataifa. Chaguo bora lilikuwa kuhamia Saudi Arabia. Wachezaji wote wanaochezea Saudi Arabia wako hapa, kwa hiyo inaleta maana kwangu kuwa hapa pia." Mukhtar Alisema.

Mukhtar hakuchelea kuisaidia Saudia kwani yeye na wenzake wa kikosi cha soka cha Saudia, waliiwezesha taifa hilo kushiriki kwenye mashindano ya Olimpiki mnamo 2021, ikiwa ni mara ya kwanza timu ya soka kufanya hivyo tangu 1996.

Ali anasema kuishi Saudi Arabia kunarahisisha kufuata dini yake.

Kuna msikiti kila mahali ninapokwenda, huwa unasikia Adhana (wito wa kusali). Ninapokuwa na mazoezi, kuna mapumziko yaliyopangwa kwa muda wa maombi. Kuomba huniletea hali ya amani, ndani na nje ya uwanja.

Mukhtar Ali

Licha ya kukikosa kikosi cha wachezaji 26 wa Saudi Arabia kwenye Kombe la Dunia lililopita nchini Qatar kutokana na majeraha, Ali amepata mafanikio mengi tayari ndani ya muda mfupi akiwa Al-Nassr aliojiunga nao kutoka Vitesse Arnhem ya Uholanzi msimu wa 2019 kwa kushinda mataji mawili mfululizo ya Saudi Super Cup.

TRT Afrika