Mchezo wa Mixed Martial Arts kuongezwa katika Michezo ya Afrika ya 2023

Mchezo wa Mixed Martial Arts kuongezwa katika Michezo ya Afrika ya 2023

Mixed Martial Arts au MMA, ni mchezo wa kupigana unaotumia mapigo huru au sanaa ya mapigo mchanganyiko
Mixed Martial Arts ni mchezo wa kupigana unaotumia mapigo huru / Picha: Reuters

Mixed Martial Arts au MMA, ni mchezo wa kupigana unaotumia mapigo huru au sanaa ya mapigo mchanganyiko.

Waandaalizi wa Michezo ya Afrika, All Africa Games ya 2023 yatakayofanyika nchini Ghana wametangaza kuwa MMA, itaongezwa katika programu pana ya michezo hiyo.

Mashindano hayo yalikuwa yafanyike Agosti lakini limeahirishwa hadi Machi 2024 kutokana na masuala ya kiuchumi na miundombinu.

Sasa MMA itajiunga na michezo ya kielektroniki (gemu) , mpira wa kasi (speedball), sambo na teqball kama sehemu ya maonyesho ya michezo.

Washindani wa MMA wataungana na michezo 15 ya Olimpiki iliyotangazwa hapo awali, mingi ambayo itatoa fursa za kufuzu kwa michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, na michezo 10 isiyo ya Olimpiki.

"Kuongeza MMA katika mpango wa michezo ni ishara chanya kwamba Afrika iko tayari kukaribisha michezo mipya na ile ambayo ina maslahi makubwa ya kimataifa," alisema Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Ghanian Ben Nunoo Mensah.

"Kuna vijana wengi sio tu nchini Ghana, lakini kote Afrika ambao wanashiriki katika MMA na michezo hii inatoa fursa nzuri ya kushuhudia wanariadha bora barani Afrika wakishindana katika mchezo huu wa kusisimua."

Habari hiyo imekaribishwa na Jumuiya ya Kimataifa ya MMA (GAMMA) ambayo ina mashirikisho 24 wanachama barani Afrika.

"Tunafuraha kabisa kwamba waandaaji wametujumuisha kama moja ya michezo ya maonyesho na tunatumai kuwa hii itakuwa chachu ya kujumuishwa katika michezo mingine mingi katika siku zijazo," Rais wa GAMMA Alexander Engelhardt alisema.

"Kazi ya shirika letu, ubora wa wanariadha wetu, uwezo wetu wa kuandaa matukio bora zaidi, na thamani ya jumuiya yetu ya kimataifa inatambuliwa na sisi kushirikishwa kwa tukio hili. Hakika litasaidia maendeleo ya mchezo wetu. "

Mtanzania Chris Tibenda ndio mbabe kutoka Tanzania wa MMA | Picha: Chris Tibenda

Michezo ya Afrika 2023 itafanyika kuanzia Machi 8-23 jijini Accra, Ghana.

MMA ni nini?

MMA au Mixed Martial Arts ni mchezo wa kupigana unaotumia mapigo huru au sanaa ya mapigo mchanganyiko.

Sanaa ya mapigo Mchanganyiko ni mchezo wa mapigano kamili unaozingatia kugonga, kugombana na mapigano ya ardhini, unaojumuisha mbinu za michezo mbalimbali ya mapambano kutoka duniani kote.

TRT Afrika na mashirika ya habari