Amane Beriso ameshinda mbio za marathon za wanawake katika Mashindano ya Riadha ya Dunia yanayoendelea Budapest, kwenye mbio zilizofanyika siku ya Jumamosi asubuhi na kumaliza vyema mbele ya bingwa mtetezi na raia mwenzake Gotytom Gebreslase.
Muethiopia huyo Amane Beriso Shankule alikimbia muda wa saa 2:24:23, huku Gotytom Gebreslase akiandikisha muda wa saa 2:24:34 naye Fatima Ezzahra Gardadi wa Morocco aliyetwaa shaba akimaliza kwa saa 2:25:17.
Uhodari wa Beriso mwenye umri wa miaka 31, ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha umweshangaza wengi haswa kwa kumaliza mbele ya Gotytom Gebreslase, bingwa anyeshikilia rekodi ya mbio za marathon kwenye mashindano ya dunia kwa wanawake, baada ya kukimbia muda wa 2:18:11 huko Oregon mwaka jana.
Lonah Chemtai Salpeter wa Israel alimaliza wa nne kwa muda wa 2:25:38, Yalemzerf Yehualaw wa Ethiopia, akimaliza wa tano kwa muda wa 2:26:13 naye Rosemary Wanjiru wa Kenya akimaliza katika nafasi ya sita kwa saa 2:26:42.