Liverpool wameshinda mechi 21 kati ya 25 katika mashindano yote chini ya Arne Slot na wana mchezo mkononi dhidi ya Chelsea. / Picha: Reuters

Liverpool ilisonga mbele kwa pointi nne kileleni mwa Ligi Kuu ya England huku kiwango bora cha Mohamed Salah kikichochea kipigo cha kukumbukwa cha 6-3 dhidi ya Tottenham Jumapili.

Salah alicheza vyema akiwa na mabao mawili na pasi za mabao huku kikosi cha Arne Slot kikisambaratisha ngome ya Spurs kaskazini mwa London.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa anakuwa mfungaji bora wa nne wa Liverpool akiwa na mabao 229.

Mabao mawili ya Salah yalimshinda Billy Liddell, huku Ian Rush (346), Roger Hunt (285) na Gordon Hodgson (241) pekee wakiwa mbele yake.

'Bidii ya hali ya juu'

Wekundu hao wanaotamba wameshinda mechi 21 kati ya 25 katika mashindano yote chini ya Slot na wana mechi mkononi dhidi ya Chelsea ili kuimarisha uongozi wao katika Ligi hiyo.

Hili lilikuwa onyesho la kushangaza la moto wa Liverpool huku Luis Diaz na Alexis Mac Allister wakifunga na kuwafanya waongoze.

Dominik Szoboszlai alinyakua bao la tatu la Liverpool na nyota wa Misri, Salah akachukua nafasi baada ya mapumziko kabla ya Diaz kufunga tena.

"Kwa dakika 60 tulifanya kila kitu tulichopaswa kufanya, tulikuwa vizuri na tukiwa na mpira. Jambo kuu ni kwamba tulijitahidi sana," Slot alisema.

'Wameishiwa na la kusema'

"Lakini lazima uwe juu ya mchezo wako kwa mchezo mzima na hatukufanya hivyo."

Uamuzi wa Ange Postecoglou kushikilia safu yake ya juu ya ulinzi, iliwasababishia adhabu kali na ikawa mara ya kwanza tangu 1997 kwa Tottenham kuruhusu mabao sita katika mchezo wa ligi ya nyumbani.

James Maddison, Dejan Kulusevski na Dominic Solanke walifungia Tottenham, lakini kipigo cha nane cha ligi msimu huu kinawaacha wakisuasua katika nafasi ya 11 huku presha ikizidi kupanda kwa Postecoglou.

Kama unataka kupuuza ukweli kwamba tunakosa kipa, mabeki wawili wa kati na beki wa kushoto na hilo haliendani na jinsi tunavyoendelea... sijui niseme nini tena,” Postecoglou alisema juu ya wakosoaji wake.

TRT Afrika