Kipa Ronwen Williams aliibuka shujaa kwa kuondoa penalti 4 dhidi ya Cape Verde/ Picha: AFP

Afrika kusini imerejea nusu fainali za Afcon kwa mara ya kwanza tangu 2000, kufuatia ushujaa wa kipa wake Williams na itakutana na Nigeria, mjini Bouake siku ya Jumatano.

Ronwen Williams aliweka historia kwa kupangua penalti 4 katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Jumamosi baada ya pande zote kutofungana dakika 120 mjini Yamoussoukro.

Ni mkwaju mmoja tu, wa Bryan Teixeira wa Cape verde uliomponyoka Williams huku Afrika Kusini nayo ikijipa magoli mawili kupitia Teboho Mokoena na Mothobi Mvala.

Williams aliondoa mikwaju ya wanasoka wa Cape verde wakiwemo Bebe, Willy Semedo, Laros Duarte na Patrick Andrade.

Williams, mwenye umri wa miaka 32, anayeichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, alikataa kujizolea sifa zote licha ya ushujaa wake na badala yake, kutoa shukrani kwa wakufunzi na watalaam wa kiufundi wa timu ya Afrika Kusini.

Ufanisi huo wa Afrika kusini imeiwezesha kutua nusu fainali yake ya kwanza Afcon tangu 2000, kipindi kinachojulikana kama siku zao za ufanisi, waliposhinda taji wakiwa wenyeji mnamo 1996, kumaliza wa pili mnamo 1998 na kisha kumaliza wa tatu mnamo 2000.

TRT Afrika na mashirika ya habari