Jamhuri ya Congo ilisema Jumatatu kuwa itafanya majadiliano na shirikisho la soka duniani FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kuondoa vikwazo vinavyozuia shirikisho lake kushiriki mashindano ya kimataifa.
FIFA, kwa kushauriana na shirikisho la soka barani Afrika, siku ya Ijumaa iliifungia Congo kutokana na baadhi ya taasisi kuingilia masuala ya soka ya taifa hilo la Afrika ya kati, jambo ambalo linakiuka utaratibu kwa mujibu wa sheria za FIFA.
Congo inakanusha hili.
FIFA imesema kuwa adhabu hiyo itaondolewa iwapo masharti kadhaa yatatimizwa, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa udhibiti kamili wa makao makuu ya shirikisho la soka FECOFOOT na maeneo mengine.
Waziri wa Michezo wa Congo Hugues Ngouelondele aliambia mkutano na waandishi wa habari kwamba serikali "itawasiliana haraka sana na viongozi wa CAF na FIFA ili kujadili kuondolewa kwa vikwazo".
Aliongeza kuwa wakati serikali inatafuta maelewano, haiwezi kukiuka kanuni zake.
Kufungiwa huko ni kutokana na mizozo ya ndani ya shirikisho la soka la Congo.
Uchezaji wa soka la taifa nchini umekuwa hauridhishi katika miaka ya hivi karibuni, alisema waziri huyo.
Taifa hilo limeshindwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya AFCON tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 2015.
Licha ya matatizo yanayokumba soka la Congo, alipuuzilia mbali madai ya serikali kuingilia masuala ya shirikisho hilo. Pia alisisitiza kuwa changamoto hizo si za Congo pekee.