Shirikisho la Soka ulimwenguni FIFA imetoa adhabu ya marufuku ya mechi mbili kwa mchezaji wa Uingereza Lauren James.
Kamati ya Nidhamu ya FIFA imetoa taarifa na kueleza kuwa imefikia uamuzi huo kufuatia ukiukaji wa kifungu cha 14 cha kanuni za nidhamu za FIFA katika mechi ya Kombe la Dunia la FIFA la wanawake England dhidi ya Nigeria.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa "adhabu hiyo itatumika kwa robo fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake na mechi itakayofuata ya kimataifa baada ya hapo."
Awali, shirikisho la soka la England, kupitia taarifa yake, imesema itaunga mkono uamuzi wa FIFA na wakati huo huo kusimama na Lauren katika hali hii.
"Tutakuwa tukimuunga mkono Lauren kwa muda wote na tutakuwa tukitoa uwakilishi kwa niaba yake. Tunaheshimu kikamilifu mchakato wa nidhamu wa FIFA na hatutatoa maoni yoyote hadi baada ya uamuzi wowote kufanywa." FA ilisema.
FIFA sasa imethibitisha kuwa pia atakosa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Australia au Ufaransa, iwapo England itafika huko, lakini itakuwa huru kushiriki katika mechi yoyote ya fainali au ya tatu.
Hatua hii ya FIFA inamaanisha kuwa, iwapo England itashinda Colombia, Lauren atakosa nusu fainali dhidi ya Australia au Ufaransa na vilevile, iwapo England itapoteza mechi yake dhidi ya Colombia, Lauren atatumikia marufuku hiyo mechi ijayo ya kimataifa ya nchi yake.