Kamati ya Nidhamu ya FIFA ilisema Jumamosi kuwa imemsimamisha kwa muda Luis Rubiales, rais wa shirikisho la soka la Uhispania, kutokana na kashfa baada ya kumbusu mchezaji Jenni Hermoso kwenye midomo baada ya ushindi wa Uhispania katika Kombe la Dunia la Wanawake.
"Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya FIFA... ameamua leo kumsimamisha kwa muda Bw Luis Rubiales kutoka kwa shughuli zote zinazohusiana na soka katika ngazi ya kitaifa na kimataifa," FIFA ilisema katika taarifa yake.
Mvutano umetokea kati ya shirikisho la soka la Uhispania, FIFA, wachezaji wa timu ya wanawake wa Uhispania na hata serikali y anchi hiyo kutokana na tukio hilo.
Serikali ilielezea awali kuwa inatafuta njia za kumsimamisha Rubiales kisheria. Serikali haina mamlaka y akumfuta kazi Rubilaes japo inaweza kupendekeza na kusubiri maamuzi ya shirikisho.
Katika taarifa, Hermoso alikanusha madai ya Rubiales kwamba busu alilompa lilikuwa la makubaliano, akiandika, "Nataka kufafanua kuwa, kama inavyoonekana kwenye picha, hakuna wakati nilikubali busu alilonipa na, bila shaka, kwa vyovyote vile sikutafuta kumuinua rais."
Kusimama naye hadi mwisho
Hata hivyo Shirikisho la Soka nchini humo limakataa kumshutumu Rubiales likisema kuwa shutuma hizo 'zimetiwa chumvi' na kugeuza kisa halisi cha kilichotokea.
Shirikisho limesisitiza kuwa litasimama na Rubiales hadi mwisho na limetishia kuchukua hatua za kisheria kumsafisha jina Rubiales.
Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumamosi, shirikisho hilo lilisema ''Tutaonyesha kuwa kumekuwa na uwongo uliosemwa kuhusu kile kilichotokea na Hermoso au watu wanaomzungumza naye.''
La Roja - Wale wekundu
Timu ya wanawake ya kitaifa ya Uhispania imetoa tangazo kuwa haitoshiriki mechi zozote za kitaifa hadi rais wa shirikisho hilo Luis Rubiales aondolewe katika nafasi hiyo.
Katika kuwajibu, Shirikisho limesisitiza kumtetea Rubiales na kuwatishia wachezaji hao kuwa itawachukulia hatua za kisheria wakisusia mechi yoyote.