Kocha wa Chelsea Mauricio Pochettino anasema "haiwezekani" kwa Chelsea kujiona kama timu dhaifu huku wakijiandaa kwa mechi ngumu ya kukabiliana na mabingwa wa Ligi Kuu ya premier league, Manchester City.
Chelsea, iliyoko nafasi ya kumi, imekuwa na rekodi mbovu hivi karibuni dhidi ya City-kwa kupoteza mechi sita zilizopita katika mashindano yote bila kufunga hata bao moja.
Hata hivyo, wanaelekea mechi ya leo Stamford Bridge wakijawa na motisha kufuatia ushindi mkubwa wa mabao 4-1 dhidi ya Tottenham wiki iliyopita.
Pochettino, akiwa katika msimu wake wa kwanza, Chelsea, alikuwa na sifa kubwa kwa kocha wa City Pep Guardiola na timu yake kwa ujumla kabla ya mechi yao jumapili.
"Kwangu mimi ni timu bora, wana kikosi bora kinachofundishwa na meneja bora," alisema. "Tunahitaji kusema ukweli-ni moja ya vilabu bora duniani.
"Unapokuwa na matokeo unayoonyesha ni kwa sababu kutoka juu hadi chini unafanya mambo kweli, vizuri sana.”
Lakini Muargentina huyo alisema timu yake imeonyesha katika mechi yao dhidi ya Spurs kwamba walikuwa na talanta na azma ya kushindana na vilabu vya juu.
Guardiola, kocha wa viongozi wa Ligi kuu ya England, Man City, amesema anahofia tishio linaloletwa Na Chelsea, ambao wanatafuta ushindi wao wa nne katika michezo sita ya ligi hiyo.
Beki wa City John Stones atakosa mechi hiyo akiwa na tatizo la misuli lakini Guardiola alisema jeraha hilo halikuwa baya kama lilivyohofiwa awali.