Sebastien Haller alifunga bao la ushindi dakika tisa kabla ya mechi kumalizika huku wenyeji Côte d'Ivoire wakinyakua taji la tatu la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Nigeria kwenye fainali kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara mjini Abidjan Jumapili usiku.
Ilikuwa ni ushindi uliotokana na misukosuko huku Wenyeji wa Ivory Coast waliposalimika kuchujwa kwenye kundi lao kufuatia vipigo viwili, kikiwemo kipigo cha aibu cha mabao 4-0 kutoka kwa Equatorial Guinea, kabla ya kupata kiwango chao katika raundi ya mtoano kwa azma kubwa ya kutokubali kushindwa iliyowapelekea kunyanyua kikombe.
Bao la kichwa la William Troost-Ekong liliipatia Nigeria bao la kuongoza kipindi cha kwanza aliporuka na kukutana na mpira wa kona wa Samuel Chukwueze, lakini Franck Kessie alisawazisha dakika chache tu baada ya kuachwa bila mlinzi kwenye eneo la hatari kwa lango.
Kitita cha zawadi
Wenyeji Ivory Coast walilazimika kutoka nyuma mara kadhaa kwenye dimba hilo na walifanya hivyo tena wakati Haller alipoelekeza krosi ya Simon Adingra wavuni, jambo lililomfurahisha sana kocha wake Emerse Fae, ambaye alianza mchuano huo kama msaidizi wa Mfaransa Jean-Louis Gasset aliyetimuliwa.
Siku ya Jumamosi, Afrika Kusini iliishinda DRC na kushika nafasi ya tatu katika michuano hiyo.
Mabingwa hao wanatarajiwa kupata dola milioni saba baada ya CAF kuongeza zawadi ya ushindi kutoka dola milioni tano walizopewa washindi wa toleo la 2022.
Washindi wa pili watapata dola milioni nne huku timu za nafasi ya tatu na nne zitapata dola milioni 2.5 kila moja.