Tanzania itamenyana na mabingwa watetezi Afrika Kusini katika michuano ya TotalEnergies CAF Women’s Africa Cup of Nations (WAFCON) Morocco 2024.
Timu ya Tanzania, Twiga Stars imepangwa Kundi C pamoja na Afrika Kusini, Ghana na Mali wakati wa droo iliyofanyika Ijumaa usiku kwenye Kituo cha Ufundi cha Mohammed VI mjini Sale, Morocco.
Tanzania iliyofuzu baada ya kuzishinda Ivory Coast na Togo itarejea WAFCON baada ya miaka 14 tangu ilipocheza mara ya mwisho kwenye michuano hiyo 2010.
Timu zote mbili, za wake na waume nchini Tanzania wamefuzu mashindano ya Afcon na Wafcon.
Waakilishi wengine wa pekee kutoka Afrika Mashariki DRC, pia wamepangwa kundi matata pamoja na Senegal, Zambia, ambao wametajw akuwa timu iliyoboreshwa zaidi na wenyeji wa shindano hili Morocco katika Kundi A.
Kundi A, inatazamiwa kuwa gumu zaidi katika shindano hili kwa hiyo DRC watakuwa na kibarua kigumu.
Nigeria, timu ambayo imetawala kombe hilo la Soka ya Wanawake wa Afrika kwa zaidi ya muongo mmoja imepangwa dhidi ya Botswana - ambayo inashiriki kwa mara ya pili, pamoja na Tunisia na Algeria.
Mabingwa watetezi wa kombe hili kwa sasa ni Afrika Kusini, japo ushindi wao wa kwanza, ilhali timu iliyo na ushindi mara nyingi zaidi ni Nigeria ambao wameshinda mara 9.
WAFCON 2024 itakayoshirikisha timu 12 itafanyika katika miji ya Morocco ya Rabat na Casablanca kuanzia Julai 5-26, 2025.
Kama ilivyo kitengo cha wanaume Afcon, zawadi za washindi pia zimeongezwa mwaka huu kwa Wafcon, ambapo Mshindi atatwaa dola 600,000, mshindi wa pili atachukua nyumbani dola 400,000, na wa tatu kupewa dola 350,000. Hata watakaoshindwa watarudi nyumbani na pesa za kutufia machozi.