Na Camille Sari
Morocco, ambayo imekuwa chini ya Mpango wa Marekebisho ya Kimuundo tangu mwaka 1983, inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii huku kukiwa na wito wa ubinafsishaji zaidi, kupunguzwa kwa matumizi ya umma na kupunguza thamani ya sarafu yake.
Hata hivyo, nchi hiyo imeorodheshwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kama mojawapo ya nchi zilizo na viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu.
Kuna mambo mengi yanayochochea maendeleo ya Morocco ikiwemo kukua kwa kiwango cha watu wazima kusoma na kuandika, mwelekeo chanya wa kiwango cha uandikishaji shuleni katika maeneo ya vijijini na pia uwekezaji katika miundombinu ya barabara, bandari na reli.
Sera ya afya ya vijijini na mijini na usambazaji mpana wa mpango wa bima ya afya umeboresha ustawi na tija ya wafanyikazi wa Morocco.
Kwa hakika, muundo wa sera ya Moroko unaokazia mauzo ya nje, pamoja na msisitizo wa biashara huria, inasaidia kuboresha uwazi wa soko la Moroko kwa ulimwengu wa nje.
Nchi inaelekea kufaidika - ndani na nje - kutokana na sera yake ya uwazi.
Morocco inategemea sana baadhi ya viwanda vya usindikaji vikiwemo vya nguo, ngozi na nyanya zinazouzwa nje ya nchi, na hilo linafanikiwa kwa kuendeleza sekta ya uzalishaji viwandani.
Hii inaipa nchi hiyo ya Afrika Kaskazini mapato ya fedha za kigeni. Baada ya uhuru wake, maendeleo ya kiuchumi ya Morocco yalilenga kwa kiasi kikubwa kujenga mabwawa na kuendeleza kilimo kwa ajili ya kujitosheleza na kuuza nje.
Hata hivyo, tangu miaka ya 2000, mapinduzi ya viwanda yamechukua nafasi, na kuvutia wawekezaji wa kimataifa ikiwa ni pamoja na makampuni ya magari.
Mkakati kabambe
Baadaye, nchi hiyo ilichukua hatua mahsusi ikiwa ni pamoja na kuendeleza viwanda, kutangaza sheria mpya za uwekezaji, kutoa motisha kwa mauzo ya nje, usaidizi kwa makampuni yanayouza nje na kurahisisha taratibu za ushuru.
Uuzaji nje wa bidhaa za viwandani umepanda kutoka 15% ya thamani yote hadi 35%, kulingana na ripoti ya ubalozi wa Ufaransa huko Rabat mwaka jana.
Uwezo wa nchi kushindana na nchi nyingine unategemea na raia wake kufaa katika soko la kimataifa la ajira, kuboreshwa kwa uzalishaji, mafunzo ya ufundi stadi, kupambana na kutojua kusoma na kuandika, pamoja na kuhimiza uvumbuzi na utafiti na maendeleo.
Serikali nchini Moroko ina jukumu muhimu katika mkakati kabambe wa maendeleo ambapo uundaji wa makampuni makubwa unalingana na changamoto zinazoletwa na miungano mikuu ya kikanda na kimataifa ya ulimwengu wa kisasa.
Nchini Morocco, makampuni mengi huwa yanachukua nafasi kubwa ya kikanda na kimataifa, kusini mwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kaskazini katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Biashara Ndogo na za Kati za Morocco (SMEs) zimejiandaa vyema kukabiliana na ushindani wa kigeni, katika soko la ndani na nje ya nchi, na kuunda makampuni yenye nguvu.
Matarajio yao ni kupata teknolojia ya kutosha, kuendeleza uwekezaji na ajira, na kusimama kama mhimili wa uundwaji wa biashara za kati na ndogo.
Ukiondoa makampuni fulani ya usindikaji yanayohitaji nguvu kazi kubwa, makampuni mengi ya Morocco yanawekeza zaidi katika uwezo wa kiufundi, kibiashara na kifedha.
Mauzo ya nje yanaongezeka
Uhamasishaji wa mtaji unaohitajika kuwekeza, mageuzi na urekebishaji mifumo umesukumwa na mabadiliko ya sekta ya benki na fedha.
Morocco iliunda ushirikiano na benki za kigeni, kuboresha sekta ya benki, mifumo ya malipo na maendeleo ya mtandao wa benki na mfumo wa usambazaji wa mikopo unaofaa kwa uwekezaji wakubwa.
Uwezo wa sekta binafsi ya Morocco kuchukua nafasi muhimu katika mchakato wa maendeleo unahitaji uchumi unaogusa sekta mbalimbali, kama vile hoteli, usafiri wa mijini, chakula cha kilimo, usindikaji na teknolojia mpya ambazo zilipata msaada kutoka uwekezaji wa kigeni katika sekta za magari, angani na dijitali.
Katika miongo ya karibuni, Morocco imepiga hatua katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la kiwango cha 7% kwa mwaka katika urahisi wa kuanzisha biashara, idadi ya ajira imeongezeka kwa 6.7% kwa mwaka na mishahara iliongezeka kwa 13% kwa mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya IMF kuhusu Moroko, mauzo ya viwanda yamekua kwa 13.5% kwa mwaka. Sehemu ya uwekezaji wa kigeni katika sekta ya viwanda imepanda kutoka 28% mwaka 1990 hadi 35% kati ya 2010 na 2020. Ripoti hio ilisema kiwango cha ukuaji wa kila mwaka katika uwekezaji viwanda kilikuwa 24%.
Kupanda kwa sehemu ya Pato la Taifa kunahusiana zaidi na sekta ya mambo ya nje, lakini pia na mienendo ya sekta zingine.
Viwanda vya usindikaji vinaendelea kulenga zaidi uzalishaji wa bidhaa za walaji, ambazo zinachukua karibu 50% ya jumla ya pato, wakati bidhaa kuu zinachukua zaidi ya 22%, kulingana na ripoti ya kila mwaka ya Benki ya Al Maghrib.
Idadi kubwa ya bidhaa zinazotengenezwa huchakatwa vizuri, na kiwango cha ongezeko la thamani kinaongezeka.
Ripoti hiyo ilisema kwa mwaka 2022, mauzo ya nje ya Moroko ya bidhaa za viwandani ilifikia euro 22 baada ya ongezeko la euro 6.272 bilioni ikilinganishwa na kiasi cha 2021.
Ilisema bidhaa zilizochakatwa kidogo zilikuwa juu kwenye orodha ya mauzo ya nje ya Moroko, na kuzalisha euro bilioni 63.88, ongezeko la euro bilioni 2.631 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2021. Kwa undani, hizi ni pamoja na mbolea za asili na za kemikali (euro 3.44 bilioni), asidi ya fosforasi (euro 1.232 bilioni) na vifaa vya kelektroniki (euro 0.35 bilioni). Zaidi ya haya ni bidhaa zinazotokana na phosphate.
Changamoto
Bidhaa za watumiaji zilizokamilika zinakuja katika nafasi ya pili kati ya mauzo ya nje ya Moroko, na jumla ya euro bilioni 61. Magari ya abiria pekee yanachangia mauzo ya bidhaa za watumiaji zilizokamilika, na kufikia euro bilioni 2.52.
Katika nafasi ya 3, vifaa vya viwandani ambazo zilichangia mauzo ya nje yenye thamani ya euro 3.59 bilioni. Bidhaa hizi ni kama nyaya na vifaa mbalimbali vya umeme.
Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia ya 2022, bidhaa za chakula zinashika nafasi ya nne katika mauzo ya nje zikichangia jumla ya euro bilioni 3.47 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka. Zinajumuisha mazao ya bahari kama na uduvi, kamba na samakigamba, nyanya mbichi na matunda yaliyokaushwa.
Vizuizi vikubwa vya uchumi wa Moroko katika ngazi ya kimataifa na kitaifa.
Hivi ni pamoja na utegemezi wa bidhaa za msingi na vizuizi vya kibishara vya wazi na visivyo vya moja kwa moja na ubaguzi dhidi ya bidhaa za Moroko zinazopelekwa Umoja wa Ulaya.
Suala jingine ni kwamba gharama za uzalishaji katika Ulaya Mashariki na Asia pia ziko chini sana.
Moroko inakabiliwa na ushindani mpya katika maeneo ambayo ilikuwa inatawala kama vile uzalishaji wa nguo.
Japokuwa inapiga hatua kubwa, ipo haja ya kukabiliana na changamoto hizi na kujaribu kuzishughulikia ili kudumisha mkondo wake wa kiuchumi.