Na Ata Şahit
Wakati Rais mteule wa Marekani akijiandaa kuingia madarakani Januari 20, 2025, eneo la Mashariki la Kati litakuwa likiujaribu utawala huo mpya, hususani suala la Iran.
Kwa sasa, ushindi wa Trump umeibua tafsiri mbalimbali ndani ya siasa za Iran na hivyo kuongeza mgawanyiko zaidi ndani ya nchi hiyo.
Wakati akiiongoza Marekani kwa mara ya kwanza mwaka 2016, Trump alilenga kuleta mageuzi kwenye masuala ya mahusiano ya kimataifa, hususani saula la Mashariki ya Kati.
Kujiondoa kwa utawala wa Trump kwenye mpango wa JCPOA, ambao ulisainiwa wakati wa Barack Obama ulikuwa na athari kwenye siasa za Iran.
Kwa mfano, baada tu ya Trump kujiondoa kwenye mkakati wa Nyuklia, wanamageuzi wa Iran walimwandikia barua Trump, wakitaka Iran ihusishwe kwenye majadiliano hayo.
Kwa upande mwingine, wahafidhina wa Iran waliutaka utawala wa kiongozi wa wakati huo, Hassan Rouhani kusitisha uhusika wa Iran katika mkakati huo.
Uhusika wa Urusi na China
Huku Trump akirudi ndani ya Ikulu ya Marekani mwezi ujao, Iran inaendelea kukabiliana na hali mbaya ya kisiasa inayotokana na tofauti za kitikadi kati wa wahafidhina na wanamageuzi.
Wanamageuzi wanakubali kuwa mkakati wa Trump wa kuidhibiti China na kupunguza uwepo wa jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati unatoa makubaliano na Iran kuwa ya kuepukika.
Kwa lugha nyingine, kukubaliana na Iran ni mpango mkakati wa kusukuma mbele ajenda ya Marekani ulimwenguni.
Ingawa makubaliano yanayoweza kutokea kati ya Marekani na Iran chini ya uongozi wa Trump yangedhoofisha uhusiano wa Tehran na Moscow na Beijing, wanamageuzi wa Iran wako tayari kucheza kamari hiyo, wakitafuta muunganiko mkubwa.
Mtazamo wa kihafidhina, hata hivyo, unasisitiza usalama wa Iran na hali iliyopo ya kijiografia, ambayo inakinzana na hesabu za serikali ya Marekani kwa vile Trump angesukuma mabadiliko makubwa katika mwenendo wa kikanda wa Iran, hasa kuhusiana na ushirikiano wa kikanda unaoungwa mkono na Iran kama vile "Mhimili wa Upinzani" katika Mashariki ya Kati.
Kujiondoa kwa Trump kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia mwaka 2016 kumeimarisha dhana miongoni mwa wahafidhina kwamba Washington upande usioaminika. Zaidi ya hayo, msimamo thabiti wa utawala wa Trump kuhusu mpango wa makombora wa Iran na ushawishi wa kikanda umeimarisha zaidi upinzani wa wahafidhina kwa mazungumzo yanayoweza kutokea.
Ni upi mkakati wa Iran chini ya utawala wa Trump?
Kwa vyovoyote vile, serikali ya Iran ina uwezekano mkubwa wa kufuata mkakati wa pande mbili - moja inayolenga kupunguza shinikizo la kimataifa kupitia upunguzaji wa hali ya kimataifa; na nyingine iliyojitolea kuimarisha ushawishi wa kikanda.
Mtazamo huu utaakisi katika matamshi ya kidiplomasia ya Tehran, ambayo yatajikita katika kuweka wazi Iran iliyo wazi kwa mazungumzo na wakati huo huo kuimarisha ulinzi wake na washirika wa kikanda ili kutopoteza mwelekeo juu ya malengo yake ya sera za kigeni.
Kwa upande mwingine, Tehran huenda ikadumisha ushirikiano wake na Shirika la kimataifa la kudhibiti nguvu za Atomiki (IAEA) , kwa kiasi, huku ikiendelea na mpango wake wa nyuklia.
Hata hivyo, huku mizozo ya kiuchumi ikizidi, Iran inaweza kutoa nafasi kwa pande zinazopingana ili kumsaidia Rais wa nchi hiyo kuungwa mkono kutoka mataifa ya Ulaya.
Hivyo, huenda Iran ikafungua baadhi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, kuwezesha ufikiaji wa mtandao wa kasi ya juu, na kuruhusu udhihirisho wa matakwa ya kidini na kikabila kwa kiwango fulani.
Kwa ujumla, nchi hiyo inaonyesha dalili za kuunda mkakati ili kulinda msimamo wake katika nyanja za sera za ndani na nje, huku ikihakikisha mpango wake wa nyuklia unaendelea hata kama Trump atarejea ndani ya Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, yote haya yatategema na namna Trump atashughulikia suala la Iran. Kwa jinsi ya hulka ya Trump ilivyo, si ajabu kuiona Tehran ikikabiliwa na vikwazo.
Mwandishi wa maoni haya, Ata Şahit ni mzalishaji mkuu wa TRT.