Alipohitimu chuo kikuu baada ya kusomea Sheria, Faraja Kotta Nyalandu, alisalia na azma moja pekee; kusuluhisha changamoto kwenye sekta ya elimu Tanzania.
Faraja, aliyeibuka na ubingwa wa Miss World Tanzania 2004, na tuzo mbalimbali za uanamitindo, alilivalia njuga suala hilo ili kuleta usawa kwenye sekta ya elimu nchini humo kupitia teknolojia.
Mnamo mwaka wa 2013, Faraja alianzisha mfumo wa Shule Direct, unaowawezesha wanafunzi na walimu kupata mtaala wa elimu kupitia vipakatilishi na simu, huku akiwaunganisha mamilioni ya wanafunzi na walimu katika kila kona ya taifa hilo na mtaala.
Kwa Faraja, uzoefu wake alipokuwa mwanafunzi, ulimpa motisha zaidi kuanzisha Shule Direct kwani yeye binafsi alinufaika na mafunzo kupitia njia ya kielektroniki iliyomrahisishia masomo yake na kumuunganisha na wanafunzi wenzake, wahadhiri, na masomo kwa jumla.
“Teknolojia ina nafasi kubwa sana katika kufanikisha malengo ya kujifunza na malengo ya kufundisha kwa walimu na wanafunzi. Shule Direct inatoa elimu kupitia wavuti na njia ya simu inayoshirikisha mafunzo kuhusu masomo mbalimbali kulingana na mtaala wa kitaifa." akieleza katika maongezi na TRT Afrika wakati wa kongamano la Next la TRT World Forum.
Licha ya kupata fursa nzuri ya masomo ya hali ya juu kuanzia jiji kuu la Dar Es Salaam, aliendeleza masomo yake nchini Uingereza hadi kuhitimu na shahada ya uzamili ya uwakili kutoka chuo kikuu cha Dar Es Salaam, Faraja hakusahau ndoto yake ya kuhakikisha kila mtoto anapaswa kupokea elimu bora zaidi.
“Elimu ni haki ya kila mtoto. Na ni lazima kila mtoto apewe nafasi,”
Kulingana na muanzilishi huyo wa Shule Direct, lengo lake kuu lilikuwa kuimarisha jamii kiuchumi na kisosholojia kwa kurahisisha uenezaji na ustawishaji wa elimu.
“Tunatumia majukwaa ya Teknolojia kutoa mitaala ya wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari ili waweze kujifunza na pia kuwapa walimu maarifa na nyenzo ili kuwa walimu bora zaidi”.
Asilimia ya idadi ya wanafunzi waliojiunga na shule ya sekondari ni asilimia 28.67 pekee.
“Leo hii mtaala ukitoka na kuchapishwa Dar Es Salaam, inachukua muda mrefu kufika kwa mfano, Sengerema. Kwa hivyo, kupitia teknolojia, mwanafunzi anapokea mtaala mpya papo hapo, masomo, mswali, mazoezi ya mtihani na kufanikisha upatikanaji.”
Mlimbwende huyo ambaye ni kitinda mimba kwenye familia yao, amejituma kujaza pengo lililoachwa na uhaba wa walimu, ukosefu wa vitabu vya shule na maktaba ya kutosha kupitia mfumo wa Shule Direct.
Aidha, uvumbuzi huo pia haujawaacha nyuma wazazi kwani umewawezesha wao pia kutumia Shule Direct kufuatilia kazi za wanao shuleni na kuwasaidia katika masomo yao pindi wanapohitaji msaada.
Kazi yake imewavutia wengi na kupokea pongezi kutoka sekta mbalimbali kwani imetegua kitendawili kilichokuwa kikiwakanganya wengi haswa elimu nchini Tanzania.
Licha ya serikali ya Tanzania kutangaza malipo ya bure kwa shule za sekondari, ripoti za awali kuhusu hali ya elimu nchini Tanzania, zimefichua kuwa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa walimu waliohitimu, Shule nyingi pia hazina vifaa kama vile vitabu vya masomo, na vifaa vingine vya kujifunza, uhaba wa madarasa na pia uhaba wa vitendea kazi.
Takriban vijana Milioni 1.5 nchini Tanzania hawapo shuleni
Aidha, shirika la Unicef, limeeleza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya watu nchini Tanzania ni watu wasiozidi umri wa miaka 18 huku nchi hiyo pia ikiwa mojawapo ya mataifa yanayoongoza kwa idadi ya vijana inayokua kwa kasi.
Ukosefu wa usawa kwenye sekta ya elimu haswa kutokana na mazingira tofauti ya kusoma pia imepelekea Baraza la mitihani Tanzania (NECTA) kuondoa uorodheshaji shule bora na mwanafunzi bora wa mtihani huo mapema mwaka huu. Kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani Tanzania NECTA Athumani Salumu Amasi, alitoa uamuzi huo.
Ingawa uvumbuzi wa Shule Direct unaonekana kuwa jambo rahisi kwa baadhi ya watu, kwa Faraja, inahusisha bidii, juhudi na wahusika wengi kuyafikisha haya masomo kwa mwanafunzi anayekabiliwa na changamoto.
Mnamo Agosti 2019, Shule Direct ilitambulika kwenye tuzo za elimu za Tanzania na kutunukiwa kuwa Mfumo Bora wa Mwaka wa Elimu Mtandaoni.
Kwa Faraja, kupitia Shule Direct, amekuwa Faraja kwa nchi yake, kwani mbali na kujaza pengo lililoko kwenye sekta ya elimu, pia amechangia pakubwa uboreshaji wa elimu kwa wasichana.
“Teknolojia hii pia imemfaa sana mtoto wa kike kwa sababu changamoto zao ni nyingi. Mtoto wa kike anakosa kufika darasani kwa majukumu ya nyumbani, wakati mwingine kutokana na ujauzito, na shida anazozipitia. Hivyo basi, Shule Direct humrahisishia kupokea mafunzo akiwa nyumbani.” Amesema Faraja.
Juhudi za Faraja hazikuambulia patupu kwani, mnamo mwaka wa 2016, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Shule Direct alituzwa kama mwanamke anayeongoza katika Teknolojia barani Afrika (Leading Women in Technology Award).
Miaka miwili baadaye, 2018, aliorodheshwa kuwa kati ya Vijana 100 wenye Ushawishi zaidi barani Afrika kutokana na mikakati yake ya kurahisisha elimu katika hafla ya tuzo za Africa Youth Awards. Pia, Jukwaa la Kiuchumi la Ulimwenguni (WEF) lilimjumuisha Faraja kuwa mojawapo wa Kiongozi Mchanga wa Ulimwenguni mnamo 2020 kuhudumu kwa muda wa miaka mitano.
Mwezi Novemba mwaka jana, alichaguliwa kuiwakilisha Afrika kwenye Bodi ya Kampeni ya Kimataifa ya Elimu.