Aerial: Menlo Park in Silicon Valley at Sunset / Photo: Getty Images

Na Mpoki Thomson

Mwaka 2019 nilihudhuria darasa la Biashara na Uwekezaji lililoandaliwa na Sahara Ventures, kampuni inayojihusisha na teknolojia, ubunifu na ujasiriamali jijini Dar es salaam. Mgeni mzungumzaji alikuwa si mwingine bali ni Mfanyabiashara muwekezaji kutoka Afrika Kusini, Vusi Thembekwayo. Kauli mbiu ikiwa ni ‘Fikra za ukuaji na Ujasiriamali’, mkutano huo uliniacha na maswali mengi pamoja kama ulivyokuwa na majibu.

Vusi kwa bashasha alielezea ikolojia mazingira ya uanzishaji biashara kwa Afrika, na kwa jinsi gani tumepiga hatua kufikia hata tulipo sasa. Aligusia mambo mengi muhimu yanayozunguka mazingira ya uanzishaji biashara, akatoa pia mafundisho aliyoyapata kutokana na kushindwa kwake na ukuaji wake.

Wakati anatushirikisha uzoefu wake, kuna kitu kimoja kilikuwa ni cha kipekee kwa wasikilizaji wake vijana wenye ndoto za kuwekeza kwenye teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ilikuwa ni jinsi ambavyo biashara chipukizi zilivyojengwa vibaya kwa kufikiri kuwa wanaweza wakaiga aina ya mfumo wa uwekezaji wa Silicon Valley.

(Silicon Valley, kusini mwa San Francisco Bay Area ya California, ni nyumbani kwa makampuni mengi ya kijasiriamali na biashara chipukizi ya teknolojia duniani)

Kitu kilichostua kutoka katika mtazamo huu tofauti wa jinsi biashara za Afrika zinavyojengwa kwa kuiga mfumo wa kimagharibi ni kwamba tumeshawahi kuwa hapa kabla na tumeona hili likifanyika sio tu katika ikolojia ya biashara chipukizi bali hata katika sekta zingine.

Afrika inang’ang’ania mitazamo na kanuni za kimagharibi ambazo ni wazi kabisa haziendani na mazingira ya bara hili. Maendeleo ambayo Afrika imeyafikia kwa miaka kadhaa sasa hasa upande wa teknolojia na maeneo mengine ya maendeleo yanadumazwa pale tunaporuhusu tamaduni tofauti kuamua namna ya uendeshaji wake kutuamulia mafanikio yake yanatakiwa kuwa vipi.

Kwa bahati mbaya, Utegemezi wa tamaduni za kimagharibi unaweza kuwa umeandaliwa kimfumo, hasa katika sekta ya uwekezaji. Mwaka 2022 Biashara chipukizi Afrika zilivutia takribani dola bilioni 5 za kimarekani, huku msaada mkubwa ukielekezwa upande wa masuala ya teknolojia.

Hata hivyo, kwa muktadha huu changamoto ni kwamba kiasi kikubwa cha msaada kilitoka katika kanuni za Kimagharibi zenye nguvu za maamuzi ya kiuchumi.

Sio siri kwamba wawekezaji wa nje wametawala uwanda wa mitaji katika bara hili, wakitoa ukwasi unaotakiwa ili kuanzisha kampuni za ndani. Kwa mujibu wa ripoti ya benki ya Afrika (African Development Bank’s (AfDB) 2021 report,) Asilimia 90 ya uwekezaji katika teknolojia katika bara la Afrika umegawanyika kati ya Kenya, Nigeria, Misri na Afrika Kusini.

Hamu ya uwekezaji wa kigeni

Kwa miaka mingi sasa, kampuni kubwa ya kimarekani ya teknolojia Google imekuwa ikitoa ukwasi huru wa mitaji kwa biashara zinazoanzishwa barani Afrika. Hifadhidata ya kila mwezi na jukwaa la utambuzi katika uwekezaji wa biashara chipukizi Afrika iliyopewa jina ‘Afrika: Jambo Kubwa’ "The Big Deal" , Inaripoti kuwa, kwa mwaka 2022 pekee, Google kwa kupitia Black Founders Fund, iliwekeza zaidi ya dola milioni 4 kwa biashara chipukizi 60 za Afrika.

Kitu ambacho kinaendelea kuibana Afrika kuendelea kuiga mfumo wa makampuni ya kimagharibi katika ufanyaji biashara na kwamba wawekezaji 6 katika 10 bora ni makampuni ya kigeni.

Hamu ya uwekezaji kwa makampuni ya nje yanavuka mipaka zaidi ya sekta binafsi. Taasisi za serikali na za kijamii nazo pia zinaonekana kuvutiwa na matokeo tarajiwa ambayo ikolojia ya biashara chipukizi inayaonesha.

Tukirudi kwa kile ambacho Vusi alitushirikisha kuhusiana na kikwazo kinachokwamisha biashara nyingi za vijana wa kiafrika, tamaa ya kukua kwa haraka kwa kuvutia wawekezaji ina mchango mkubwa sana kwa mtaalamu wa uwekezaji, ambaye amepita kwenye milima na mabonde ya biashara, anaamini kwamba suluhisho la uwekezaji na biashara Afrika lipo ndani ya hili bara na utayari wake wa kufungua njia zake za kibiashara.

Anapigia chapuo Afrika isiyo na mipaka ambapo biashara ya ndani haizuiliwi na changamoto za kiushuru au zile ambazo si za kiushuru.

Ukiweka katika muktadha wa Afrika ya kisasa kuamua hatma yake, wazo hili linafungua mjadala mwingine wa kwa nini bara hili limeshindwa kujikwamua kutoka mikononi mwa wakoloni.

Mpaka leo Afrika bado inafuata maelekezo na maagizo ya mataifa yenye nguvu ya magharibi. Toka kwenye mtazamo wa kimazingira na kijamii mpaka kwenye mtazamo wa kiuchumi, tunaendelea kutegemea masuala ya nje ili kusonga mbele ambako kunaendana na stori yetu ya mafanikio na hatam yetu kwa ujumla.

Kwa hiyo, Mjasiriamali aliyefanikiwa anaposhirikisha mawazo yake ambayo yanaweka wazi ukweli wa bara la Afrika kutegemea misaada ya wahisani. Ni kama anatoa mwangwi wa maneno ambayo yamekuwa yakizungumzwa tangu kale “Afrika inatakiwa kumiliki hatma yake.”

Udhaifu kwa Afrika

Jumanne Mtambalike | Picha: Jumanne Mtambalike

Makampuni makubwa kama Google kwenye huu ulimwengu daima wataweka mbele maslahi yao kwa kuangalia fursa zinazowanufaisha zaidi. Kwa asili ya ulimwengu, Wenye nguvu hupanua wigo wa milki zao. Je, tupo tayari kubadili mwenendo wetu wa maisha na jinsi ya kufikiri ili kuendana na nini ambacho ni kizuri kwetu na ambacho sicho?

Hii tu pekee ni aina ya kutiishwa ambayo inawanyima wanaume na wanawake wa Kiafrika utambulisho wao.

Tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe na bara ambalo ndio tunaliita mama yetu kama tutashindwa kukubali kwamba Afrika ni tofauti ukilinganisha na pande nyingine za dunia. Kuna sababu ambayo inafanya leo hii tuainishwe kwamba sisi ndio kesho ya ulimwengu huu. Kuna sababu kwa nini mabara mengine yanakimbilia Afrika ili kujihakikishia kesho yao.

Mara tutakapostuka kwamba hali zetu zinafanana, tutakumbatia tofauti zetu ambazo zinaendelea kutengeneza na kutofautisha utu wetu na uwezo wetu halisi.

Mpoki Thomson ni mwandishi wa habari za mtandao mwenye makazi yake Dar es Salaam

TRT Afrika