Na Sylvia Chebet
Kila sekunde 30 duniani kote, mtu hupoteza maisha kwa ugonjwa unaohusiana na homa ya ini. Licha ya takwimu hizi za kutisha, viwango vya upimaji wa Homa ya Ini bado ni vya chini,' hepatitis'.
Hepatitis ni kuvimba kwa ini, ambayo mara nyingi husababishwa na maambukizi ya virusi.
Kuna virusi kuu tano za hepatitis, zinazojulikana kama aina A, B, C, D na E.
Ugonjwa huu huathiri watu na jamii zinazoishi katika maeneo yenye mifumo duni ya kiafya.
Shirika la Afya Duniani (WHO), Afrika CDC na Muungano wa Hepatitis Duniani, miongoni mwa washirika wengine wamekuwa wakiendesha kampeni iliyopewa jina la ‘Usingoje’ ili kuwafanya watu wengi kupimwa Hepatitis iwezekanavyo.
Mambukizi ya kurejea
Sudan Kusini imerekodi visa vya Hepatitis E mara kwa mara tangu 2014, na milipuko ya mara kwa mara ikitokea Bentiu, kaskazini mwa nchi, ambapo kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) ipo.
Virusi vya Hepatitis E, vinavyosambazwa kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa, vimeenea hasa katika kambi za watu waliohamishwa, kutokana na huduma duni za usafi wa mazingira.
Inaweza kusababisha ugonjwa mbaya na ni mbaya sana kwa wanawake wajawazito.
Madaktari wasio na mipaka, MSF, walitoa chanjo dhidi ya virusi kwa mara ya kwanza mnamo Julai 2022, na kuleta matumaini kwamba maambukizi mapya ya HEV na vifo vinaweza kuwa historia hivi karibuni.
Homa ya ini ya kudumu na hepatitis C pia ni magonjwa ya kuambukiza yanayohatarisha maisha ambayo husababisha uharibifu mkubwa wa ini, saratani, na kifo cha mapema.
Mara nyingi maambukizo huwa kimya na hayajidhihirishi hadi yamefikia hatua ya saratani ya msingi ya ini.
Maambukizi ya juu zaidi
Ulimwenguni, watu milioni 354 wanaishi na virusi vya hepatitis B au C.
Kanda ya Afrika ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya homa ya ini (HBV) kwa asilimia 7.5, huku watu milioni 82.3 wanaishi na maambukizi ya muda mrefu ya HBV, kulingana na shirika la WHO.
"Wawili kati ya watoto watatu walioambukizwa HBV duniani kote wanazaliwa barani Afrika. Maambukizi ya HBV yanayopatikana wakati wa kuzaliwa au utotoni ni sababu kuu ya saratani ya ini katika utu uzima," Africa CDC ilisema katika tovuti yake.
Inapendekezwa kuwa chanjo ya kawaida ya homa ya ini kwa watoto wote wanaoanza na dozi ya kwanza ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa itolewe.
Dozi mbili au tatu za ziada zinahitajika ili kukamilisha mfululizo wa chanjo ya watoto wachanga.
Kufikia 2022, ni Nchi 18 tu kati ya 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, zikiwakilisha 33% zilikuwa zimeanzisha chanjo dhidi ya virusi vya Hepatitis B.
AU ilipitisha tamko la Cairo kuhusu homa ya ini ya virusi barani Afrika mnamo Februari 2020.
Hati inayotaka kukomeshwa kwa virusi vya homa ya ini ya B na C katika bara hilo, inatarajiwa kuchochea hatua za afya ya umma kufikia kutokomeza homa ya ini ifikapo mwaka 2030.