Na Halima Umar Saleh
Kumekuwa na ongezeko la dhoruba za mchanga ambazo huzikumba sehemu za Afrika. Dhoruba hizo zinaongezeka kiwango cha ukubwa na idadi na hivyo kulizidishia masaibu bara ambalo tayari linapambana na majanga ya asili kama vile ukame, ongezeko la joto, mafuriko makubwa, vimbunga vya kitropiki na kuongezeka kwa viwango vya bahari. Matokeo yake ni ukatili wa kupotea kwa maisha, uharibifu wa mali na uhamaji wa watu
Dhoruba mchanga ya hivi karibuni zaidi imepiga nchini Cameroon mwezi wa Februari, huku wingu kubwa la vumbi kutoka Jangwa la Sahara likikumba sehemu kubwa ya nchi, hasa sehemu za kaskazini.
Kwa mujibu wa Waziri wa uchukuzi wa nchi hiyo, Ernest Ngalle Bibehe, "nusu ya nchi" ilikabiliwa na ghadhabu ya dhoruba zilizotatiza usafiri na kuchochea magonjwa ya kupumua katika maeneo yaliyoathirika.
Ramat Hassan, mvuvi mwenye umri wa miaka 23 kutoka mji wa Darak katika wilaya ya Maroua katika Mkoa wa Kaskazini wa Mbali nchini Cameroon, anaikumbuka jinsi hali ya "kutisha" wakati dhoruba ya mchanga ilipowaswaga yeye na wenzake.
"Dhoruba ilikuja ikisukumwa na upepo mkali, kila kitu mahali pote kilikuwa kimefunikwa na vumbi zito. Kulikuwa na giza nene. Hatukuweza hata kuona mto ambao tulikuwa tukivua samaki," anaiambia TRT Africa.
Hassan na wavuvi wenzake walifanikiwa kupata njia ya kurejea nyumbani kutoka mtoni, lakini baadhi yao walikuwa wamekwama na hawakuweza kurejea hadi siku iliyofuata.
“Mbaya zaidi dhoruba hiyo ya mchanga ilisababisha mafua na kikohozi kwa watu wengi, nikiwemo mimi mwenyewe,” anasema.
Sehemu za kaskazini mwa Nigeria pia zilikumbwa na dhoruba ya mchanga mwaka jana, na kukwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Ingawa hakukuwa na takwimu rasmi za majeruhi wakati huo, baadhi ya wakazi wa Borno, jimbo la kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, wanasema dhoruba hiyo ya mchanga ilikuwa nzito kiasi kwamba ilizidisha hali ya wale walio na pumu, magonjwa ya koo na upumuaji, ikiwa ni pamoja na saratani ya mapafu, na kusababisha maambukizi. kati ya watoto na wazee.
Mnamo Juni 2018, dhoruba ya mchanga katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliathiri nchi nyingi kama Chad, Niger, Mali, kaskazini mwa Nigeria, Benin, Ghana, Ivory Coast na Burkina Faso. Mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Bauchi. "Watu wengi walidhani ulikuwa mwisho wa dunia," Malam Aminu Makama, mkazi wa eneo hilo, anaiambia TRT Afrika.
Makama anakumbuka tukio hilo lilitokea siku moja baada ya Eid-ul-Fitr. "Nyumba nyingi na majengo yaliharibiwa; miti mikubwa iling’oka pamoja na mizizi yake, na magari mengi yalipata ajali mbaya," anasema.
"Mamlaka ziliripoti kuwa ni watu wawili tu waliopoteza maisha, lakini kusema kweli, tuliona watu wengi wakifariki. Baadhi ya watu walifukiwa chini ya vifusi vya majengo."
Nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati pia hukabiliwa na tatizo hili mara kwa mara. Iraq, kwa mfano, ilikumbwa na dhoruba za mchanga mara nane kati ya Aprili hadi Mei 2022, na kupelekea mamia ya watu wakilazwa hospitalini na kulazimisha safari za ndege kusitishwa.
Dhoruba za mchanga hutokeaje?
Wanasayansi wanafafanua kuwa dhoruba za mchanga ni dhoruba ambazo kwa kawaida hutokea wakati upepo wenye kasi kubwa hubeba mchanga mwingi na vumbi kutoka kwenye ardhi tupu hadi kwenye angahewa, na kuusafirisha umbali wa kilomita kadhaa. Ni majanga ya kawaida ya tabianchi ambayo hutokea katika maeneo kame na nusu jangwa.
Kulingana na Dk Bindowo Aboubakari, mwanamazingira wa Cameroon aliyebobea katika mabadiliko ya tabianchi, anasema dhoruba kawaida hutokea kufuatia "tofauti za mrindimo wa joto katika hewa".
Hii ina maana hali fulani hukoea pale ambapo makundi mawili ya hewa, yenye sifa tofauti, ikiwa ni pamoja na hali ya joto na maji, "yanakabiliana na kusababisha upepo ambao unaweza kuwa mkali sana". Kawaida huacha uharibifu mkubwa katika njia yao.
Mohammed Jafaru Dankwabia, naibu mkurugenzi wa utafiti katika Kituo cha Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Usalama wa Chakula nchini Ghana, anasema wingu la upepo ambalo linakuja na vumbi linalotembea kwa kasi karibu kilomita 70-100 kwa saa "ni jambo ambalo linahitaji kuwa na kuzingatiwa".
"Kutokana na jinsi dhoruba hii ya mchanga inavyofunika Afrika yote kutoka kaskazini, kati, magharibi na maeneo mengine kadhaa katika bara sio jambo la kupuuziwa," anasema Dankwabia.
Kwa dunia nzima, hasara itokanayo na dhoruba za mchanga ni takriban $3.6 trilioni, kulingana na Benki ya Dunia.
Kitu gani kinasababisha dhoruba za mchanga barani Afrika?
Wataalam wanalaumu matukio haya ya hali mbaya ya hewa kwa sehemu juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Dk Bindowo Aboubakari, mwanamazingira wa Cameroon anayeangazia mabadiliko ya hali ya hewa, anaiambia TRT Afrika kwamba "ongezeko la joto duniani husababisha kuongezeka kwa mzunguko na ukubwa wa dhoruba barani Afrika, ambayo huzidisha matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi katika bara".
"Dhoruba za mchanga ni kati ya matukio ya asili yenye uharibifu mkubwa na yasiyotabirika," anaelezea.
Wataalamu wanasema eneo la nchi na maeneo yaliyoathiriwa katika Jangwa la Sahara pia ni maeneo hatarishi. Sababu nyingine ni pamoja na ukataji miti na mmomonyoko wa ardhi, ambao wote huacha maeneo mengi bila kufunikwa na miti.
"Wengi wetu tunaona mabadiliko ya tabia-nchi kuwa ni matokeo ya sababu za asili," Dankwabia anasema. "Lakini mengi ya sababu hizi ni za shughuli za maendeleo na athari za moja kwa moja za shughuli za binadamu ambazo watu hawazingatii sana."
Hatua za kuchukua
EcoMENA, mpango unaoendeshwa na watu wa kujitolea wa kujenga uelewa mkubwa wa mazingira na kukuza uendelevu duniani kote, inaamini athari za dhoruba za mchanga na vumbi zinaweza kupunguzwa kwa kutumia hatua za kiafya na kiusalama, pamoja na mikakati ya kudhibiti mazingira. Moja ya hatua, inasema, ni kuongeza uoto popote inapowezekana barani Afrika.
"Uoto au mimea husaidia katika kuimarisha udongo na kuunda matuta ya mchanga ambayo hutumika kama vizuizi vya upepo," wanaeleza.
Wataalamu pia wanaamini kutumia mimea na miti asilia kama kizuizi kunaweza kupunguza kasi ya upepo na kuhama kwa mchanga huku kikiongeza unyevu wa udongo kwa wakati mmoja.
Nchi za Kiafrika kama Ethiopia tayari zimeanzisha mipango kama hii. Mnamo Julai 2019, Serikali ilitangaza kuwa miche milioni 350 ilipandwa ndani ya siku moja, kama mojawapo ya dhamira yake ya kulinda mazingira.
Mataifa mengine mengi ya Kiafrika yalichukua jaribio la Ethiopia la upandaji miti kwa wingi ili kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa. Dankwaiba anashauri nchi za Afrika kuongeza juhudi za kupanda miti mingi na kuilinda. "Hiyo itatumika kama kizuizi cha upepo wakati jua linaposonga kutoka eneo la Sahelian. Bila vizuia upepo, hatutaweza kupunguza makali ya dhoruba za mchanga," anasema.
Sera za Miundombinu
EcoMENA inadokeza kuwa ni muhimu kubuni majengo ipasavyo na kufanya upimaji wa namna upepo unapita katika majengo hayo wa kutoa vibali, hasa katika maeneo ambayo yanaweza kukumbwa na dhoruba za mchanga.
Mbali na kuwekeza katika mifumo ya utajoaji tahadhari mapema, Benki ya Dunia inasema Serikali duniani kote zinapaswa kubuni sera za kupunguza athari za dhoruba za mchanga na vumbi, katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Kongamano la 15 la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani lilizindua mfumo wa tahadhari za dhoruba ya mchanga mwaka wa 2007 kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi kutoa utabiri sahihi na kwa wakati kupitia ushirikiano wa kimataifa wa jumuiya za utafiti na uendeshaji.
Elimu juu ya mabadiliko ya tabianchi
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi Dankwaiba anaamini kuwa elimu ndiyo msingi wa kuwafahamisha watu madhara ya mabadiliko ya tabianchi. "Mpango Mkakati wa kubadili hali hii lazima isiwe maneno tu, bali lazima ije na vitendo," anasema.
Ingawa Afrika ni mojawapo ya kanda zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa, bado kuna uelewa mdogo kuhusu hilo miongoni mwa wakazi katika bara zima. “Elimu ni moja ya mambo ambayo tunapaswa kuyapa kipaumbele ili kujaribu kuwajulisha watu hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi,” anasema Dankwaiba.
"Wakati watu watakapoelewa hili, tutaanza mpangokazi kama vile kuweka upya mazingira yetu yaliyopotea, kuenea kwa jangwa na ukataji miti, ambayo imekuwa msingi wa tatizo hili."
Anatoa wito kwa juhudi za kimataifa kupunguza athari za dhoruba za mchanga na majanga mengine ya kimazingira barani Afrika. "Bila ya kupunguza athari hizi za mabadiliko ya tabianchi, bila shaka kutakuwa na athari kwa usalama wa chakula duniani."
Hatua za kujilinda kibinafsi
Wataalamu wanasema kuwa mbali na hatua za kulinda mazingira, wakazi wanapaswa pia kuchukua hatua za kujikinga inapotokea dhoruba za mchanga.
Aboubakari anatetea hatua rahisi kama vile uvaaji wa barakoa ili kuchuja vihatarishi vidogo vinavyoweza kuingia kupitia mdomo, pua na macho.
"Ni vyema kutafuta mahali pa kujikinga kukitokea dhoruba ya mchanga. Nenda mahali kwenye miinuko kwa kuwa mchanga mwingi uko karibu na ardhi. Hii ni muhimu ili kuepuka kupigwa na vitu vinavyobebwa na upepo," anashauri.