Waandishi waliogoma ambao hatua yao ilipoozesha eneo la Hollywood, wametangaza kufikia makubaliano "ya kipekee" na studio hizo na kuongeza kuwa kuna uwezekano wa kurudi kazini.
Mafanikio dhahiri ya siku ya Jumapili yanaongeza matumaini kwamba waigizaji wanaoandamana wanaweza pia kufikia makubaliano na studio kumaliza mkwamo wa miezi mingi ambao umekwamisha uzalishaji wa filamu na Televisheni kwa kiasi kikubwa, na kugharimu uchumi wa California mabilioni ya dola.
Mgomo wa waigizaji
Maelfu ya waandishi wa filamu na televisheni waligoma mapema mwezi Mei kwa madai mbalimbali yakiwemo malipo bora kwa waandishi, malipo bora zaidi kwa kuzalisha maonyesho ya kuvutia na ulinzi kutoka kwa akili bandia.
Waandishi hao wanadai kuwa mapato yao hayajaboreshwa licha ya mfumuko wa bei, na kwamba kuongezeka kwa utazamaji wa filamu kumewageuza kuwa kama "maganda" ya karanga licha ya maonyesho wanayofanya kuvutia wengi.
Waandishi hao pia wametaka kuzuiwa kwa matumizi ya akili bandia, ambayo wanasema yanaweza kutumika kujaza nafasi zao katika kuzalisha filamu za baadaye au maandishi ya filamu, na kwa hivyo kupunguza zaidi mapato yao.
Waandishi hao walikuwa wakiandamana nje ya ofisi za Netflix na Disney kwa miezi kadhaa huku wakijiunga na waigizaji katikati ya mwezi Julai, na kuiacha Hollywood, iliyozoeleka kuwa na shughuli nyingi kila siku, kuwa tupu, kama njia ya kudhibitisha nguvu na umoja wao.