Kama umekuwa makini kufuatilia mambo mwaka huu, bila shaka utakuwa umeona mabadiliko mengi yaliyofanywa na rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika safu yake ya uongozi – hii ni kuanzia mabadiliko ya baraza la mawaziri hadi wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali.
Mabadiliko haya yamekuwa yakifanyika mara kwa mara na ndani ya mufa mfupi katika kipindi cha mwaka mmoja. Ingawa katiba ya Tanzania, inampa mamlaka kamili rais kuteua na kutengua, lakini kasi yake ya uteuaji na utenguaji ndiyo inayoibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi.
Wataalamu wa masuala ya uongozi wanaitetea hatua hiyo ya rais, na kusema kuwa, rais ni kama kocha wa mpira, anauwezo wa kubadilisha safu yake wakati wowote anapohisi kufanya hivyo kutaleta ufanisi wa utendaji wa serikali yake.
Hata hivyo, maswali mingi pia yanaibuka pale mtu mmoja anapotenguliwa zaidi ya mara moja, na baadae kuteuliwa tena katika nafasi hiyo hiyo.
Mathalan, mwezi Septemba mhandisi Peter Ulanga yalimkuta ya kutenguliwa na baada ya siku mbili kuteuliwa tena katika nafasi hiyo hiyo. Watu walimaka, lakini rais alijitetea kwa kusema kulikuwa na kosa la utafiti duni uliofanywa na timu yake ya washauri.
Mwenendo huu, unaonekana kuanza kujenga khofu miongoni mwa watumishi wa umma. Rais Samia mwenyewe anakiri katika hilo, lakini anagongea msumari kwa kuwataka viongozi wazembe kukaa chonjo.
Lakini pia, pangua pangua hii inaweza kuwa ya kimkakati. Rais anaimarisha safu yake wakati nchi ikijiandaa na uchaguzi wa serikali za mtaa unaotarajiwa kufanyika mwakani. Tupe maoni yako kuhusu haya yanayojiri.