David Beckham afichua yote katika safari yake ya soka kupitia filamu yake ya Netflix. Picha: Getty

Nyota wa zamani wa Manchester United David Beckham hii leo ameachia filamu mpya kwenye Netflix inayoangazia safari ya maisha yake ikiwa ni miaka kumi tangu alipostaafu soka.

Filamu hiyo imefichua malezi ya Beckham, uchumba wake na mkewe na ushindi wake uwanjani. Hata hivyo, sehemu inayoonekana kuwa ngumu zaidi katika filamu ilikuwa ni kurudia kuangalia kuondolewa kwake uwanjani kwa uchungu wakati wa mechi ya Kombe la Dunia ya England dhidi ya Argentina.

David Beckham na familia yake. Picha: Getty

David Beckham na mkewe Victoria Beckham, pamoja na wanao Romeo Beckham, Cruz Beckham, Harper Beckham, na Brooklyn Beckham wakiwa na Mia Regan na Nicola Peltz walihudhuria uzinduzi wa filamu ya "Beckham" Katika Curzon Mayfair, London, Uingereza mnamo Oktoba 3, 2023.

Sehemu ya kwanza ya filamu hiyo iliyozinduliwa leo Oktoba 4, inaangazia malezi ya David Beckham akiwa mchanga huko Chingford, Essex, na uhusiano wake na baba yake.

Sehemu ya tatu na nne ya filamu inaangazia tofauti yake na kocha Alex Ferguson, kuuzwa kwake hadi Real Madrid na madai ya majarida kuhusu uhusiano wake wa nje ya ndoa.

Aidha, filamu hiyo imepata umaarufu zaidi kutokana na mchango wa watu maarufu waliohojiwa kama vile Alex Ferguson, Eric Kantona, Diego Simeone, Luis Figo, Fabio Capello, Gary Neville na wengine wakitoa ufafanuzi zaidi ya David Beckham.

David Beckham alikuwa zaidi ya mchezaji wa soka, akiwa na ushawishi mkubwa wa kitamaduni na mjasiriamali. Alifanya ushirikiano na mashirika makubwa kama Adidas, Armani, Breitling na zaidi haswa katika kipindi ambacho wachezaji hawakuwa wakifanya mikataba kama hiyo. Beckham alisema kuwa hayo yaliwezeshwa na mafanikio yake kwenye uwanja wa soka.

David Beckham na Lionel Messi wakati wa uzinduzi wa Messi katika klabu ya Beckham ya Inter Miami. Picha: Getty

"Sikuzote nilihakikisha kwamba chochote nilichokuwa nikifanya nje ya uwanja hakikuathiri kile nilichokuwa nikifanya uwanjani kwa sababu hicho ndicho nilichopenda na kile kilichokuwa muhimu kwangu,” Beckham alisema.

Beckham alilishwa kadi nyekundu kwa kumpiga makusudi kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone ambaye wakati huo alikuwa nahodha wa Argentina kwa kumsukuma chini. Hilo lilivun ja Matumaini ya kombe la dunia ya England, na Beckham kugeuka haraka kutoka shujaa hadi hasara.

"Je, ningependa mambo yasingetokea? Kabisa. Je, ningependa '98 isingetokea? Kabisa.” "Lakini ilinifanya niwe na nguvu kama mtu, kama mchezaji, kama mwanadamu, na kama baba kama mume," alisema. "Na kama hilo lisingetokea, labda nisingekuwa na kazi niliyokuwa nayo.”

Beckham alisema kuwa walifanikiwa kuweka uhusiano wao na Victoria Beckham kuwa wa siri kwa miezi michache ya kwanza na kisha "mambo yakafichuka.”

Filamu hiyo ya 'David Beckham' yenye sehemu nne, ilichukua miaka minne kukamilika huku ikiishia na sehemu ya mechi ya kwanza ya ushindi wa kwanza wa Lionel Messi akiwa Inter Miami ya Beckham.

Pia, ilichukua zaidi ya masaa 45 ya mahojiano yaliyokusanywa kwa kipindi cha miaka miwili.

AP