Kampuni ya Google yapigwa faini ya dola milioni 160 kwa kutawala soko nchini India

Kampuni ya Google imepigwa faini ya dola za kimarekani milioni 160 baada ya kugundulika kuwa imesanidi mtandao maksudi ili kuwafungia washindani nchini India.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu California inatawala soko la India huku watumizi wa simu za kiganjani takriban asilimia 95 wakifurahia huduma zake.

Hatahivyo Tume ya kudadisi ushindani nchini India inasema kuwa Google imesanidi mtandao wake kwa lengo la kuwafungia washindani hasa kupitia mtandao wa YouTube na Chrome.

“Hatua ya kusanidi Google imefanywa maksudi ili kuwazuia watumiaji wa simu kupata huduma mbadala,” taarifa ya tume inasema.

“Soko linapaswa kuwa huru kwa kila mtoaji huduma.” Tume hiyo inaongeza.

Tume hiyo sasa kutokana na uchunguzi wake imeipiga Google faini ya rupee bilioni 13.4 sawa na dola milioni 162 kwa kuwalazimisha wamiliki wa simu kupakia app za Google.

Aidha pia tume hiyo imeonya Google dhidi ya kufikia makubaliano na kampuni za utengenezaji simu zilizo tayari kupakia huduma za Google kwenye simu wanazotengeneza.

Taifa la India ni la pili kwa idadi ya wamiliki wa simu za kiganjani baada ya China huku soko la simu hizo likiongezeka kwa asilimia 27 mwaka 2021 kwa mujibu wa ripoti ya Counterpoint.

Aidha zaidi ya asilimia 60 za simu zinazotumiwa India zimetengenezwa na kampuni za China Xiaomi na Oppo.

Kampuni ya Apple bado haijafanikiwa kaisa kupenyeza soko la India lakini majuzi tu ilitangaza kuwa simu ya iPhone 14 huenda ikaundiwa India.

AFP