Rais Murmu anaandaa mapokezi kwa viongozi wa G20 kwa minajili ya mkutano wa kilele wa kundi hilo utakaofanyika Jumamosi, na mialiko ilitumwa kutoka ofisi yake.
Awali India iliitwa Bharat, Bharata, na Hindustan Kabla ya ukoloni, ambayo ni majina yake katika lugha za Kihindi ambayo yanatumiwa kwa kubadilishana na umma na rasmi.
Hata hivyo, kwa kawaida Ofisi za ngazi za juu nchini humo zimeshikilia mataji yao kama vile Rais wa India, Waziri Mkuu wa India na Jaji Mkuu wa India haswa katika mawasiliano yao kwa Kiingereza.
Kwa miaka mingi serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi wa chama cha (BJP) Bharatiya Janata Party imekuwa ikiyaondoa majina ya kikoloni kwa kile inachosema, kusaidia India kujiondoa kutoka minyororo ya utumwa.
Waungaji mkono mabadiliko ya jina kama ilivyoonekana katika mwaliko huo, walisema watawala wa kikoloni wa Uingereza walibuni jina India ili kuzamisha Bharat na kutengeneza urithi wa Uingereza.
"Jina la nchi yetu ni Bharat na hatupaswi kuwa na shaka juu yake," Rajeev Chandrasekhar, Naibu Waziri wa Shirikisho alisema.
Ukosoaji
Hata hivyo viongozi wa upinzani walikosoa mabadiliko hayo huku baadhi wakisema yanalenga kuufunika muungano wao wa kisiasa uliodumu kwa miezi miwili ambao pia unaitwa "INDIA".
"Sote tunasema 'Bharat', ni nini kipya kwenye hili? Lakini jina 'India' linajulikana kwa ulimwengu... Ni nini kimetokea ghafla hadi ikabidi serikali kubadili jina la nchi?" Alisema Mamata Banerjee, mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani.
Aidha, Shashi Tharoor wa chama cha upinzani cha Congress alichapisha kwenye mtandao wa X, ambayo hapo awali ulijulikana kama Twitter, "Natumai serikali haitakuwa mshenzi kiasi cha kuachana na India, ambayo ina thamani isiyohesabika ya chapa iliyojengwa kwa karne nyingi."
Mabadiliko hadi jina "Rais wa Bharat" yanakuja chini ya miezi miwili baada ya vyama vya upinzani kuunda muungano wa "INDIA" ili kupinga BJP katika uchaguzi wa kitaifa mwaka ujao.
INDIA, kulingana na wanavyosema, inawakilisha Indian National Developmental Inclusive Alliance.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema kuwa hatua hiyo ilikuwa ubunifu wa busara wa kukabiliana na muungano wa kitaifa wa BJP.
Rais wa India ni mtendaji asiye wa chama na mwenye mamlaka yasiyokuwa na majukumu makubwa. Kijadi, anaungwa mkono na kuchaguliwa na chama kilicho madarakani.
Hata hivyo baada ya kusailiwa na Reuters, afisa katika ofisi ya rais alisema hawakutaka kuzungumzia suala hilo.