Ni wazi kuwa neno 'Islamic Banking' linatajika zaidi nchi za Afrika Mashariki miaka ya hivi karibuni.
Nchini Uganda, Benki ya Taifa imetangaza wiki hii kuwa imetoa leseni ya kwanza ya huduma ya benki ya Kiislamu nchini humo.
Mjadala mara umeibuka hasa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakishauriana kupendekeza kuhamia mfumo huo wa benki.
Hii ni kutokana na imani kuwa 'Islamic Banking', au Benki zinazotoa huduma kwa maadili au sheria za Kiislamu zinatoa huduma kwa bei nafuu kutokana na kuondolewa riba au kutozwa riba ya chini zaidi.
''Kilichonivutia kutafuta Islamic Banking, ni kuwa ni benk ya Kiislamu na haikuwa na riba," anasema Mohammed Otweyo, kutoka Nairobi, Kenya. ''Nilijua watafuata maadili na itakuwa na uaminifu, kwa hiyo itanifaa kama Muislamu,'' anaongeza.
Kwa miaka sita, Mohammed alijaribu huduma mbali mbali za benki aliyojiunga nayo. Lakini anasema alipigwa na mshangao.
''Wanasema kwamba hawana riba. Kwamba ukichukua mkopo, hautalipishwa riba,'' Mohammed anaambia TRT Afrika. '' Lakini ukiangalia utakuta kuna ada wanayotoza wanayoita faida. ukipiga hesabu hiyo faida ndio ile ile riba katika mabenki mengine ya kawaida.''
Mohammed hawezi kulaumiwa kwa kutaka kupata nafuu katika ada ya huduma za benki.
Kiujumla watu wengi kote duniani wamepoteza imani na mabenki ambayo mara nyingi yanatazamiwa kama yanalenga kumfinya mteja wao na kumkamua faida kwa njia zozote.
Lakini wataalamu wanaonya kuwa japo Benki hizi zinafuata maadili ya kiislamu, lengo kuu hasa ni kuwa 'halali,' sio kuwa ya gharama ya chini.
''Wanaoendana na huduma hizi za mabenki yanayotoa huduma za kiislamu ni wale ambao wanasema hawataki riba au kingine chochote cha haramu kwa mujibu wa kiislamu,'' anasema Mohammed Issa, mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini Tanzania.
''Tatizo linakuja pale wateja wa mabenki haya wanapodhani kwa kuwa zinaitwa huduma za benki za Kiislamu, zitakuwa nafuu zaidi au zitakuwa bure, na yale makato ya benki hayatakuwepo. Huu mtazamo sio sawa kabisa. Hizi huduma sio sadaka.'' anaeleza Issa.
Huduma za kibenki za kiislamu ni huduma zinazozingatia kanuni za kifedha za Kiislamu ambazo zinakataza utozaji na upokeaji wa riba. Lakini pia inahitaji kuweka wazi kinachoingia kimkataba kati ya benki na mteja wake, na kuhusu mambo ya haramu, katika uwekezaji kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kiislamu.
Haya ni mambo yanayotambulika rasmi na kuidhinishwa na taasisi kubwa za kifedha duniani kama vile Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani, Umoja wa Mataifa na Shirika la Maendeleo katika Umoja wa Mataifa au hata Umoja wa Ulaya.
Nchi nyingi duniani zimeratibisha mfumo huu wa utoaji wa huduma za benki za Kiislamu.
Hii ni kwa sababu huduma za Benki ya Kiislamu hazilengi waislamu pekee. Ni huduma iliyo wazi kwa yeyote anayependelea huduma hizo.
''Utaona nchi kama vile Uingereza imepiga hatua kubwa zaidi za utoaji wa huduma za kifedha za Benki ya Kiislamu kuliko nchi nyingine yoyote nje ya nchi za Kiarabu,'' Mohammed Issa anaambia TRT Afrika.
''Lakini pia mwaka 2009, papa Mtakatifu Marehemu Benedict wa kumi na sita alihimiza benki zitumie huduma za kibenki za Kiislamu ili zipate kurudisha imani na wateja wao kutokana na kuzidi riba kupindukia,'' anaongeza.
Issa ametaja nchi kama Malaysia ambayo mwaka jana 30% ya wateja wa benki za huduma ya kiislamu hawakuwa waislamu. Afrika Kusini, Tanzania, Kenya au hata sasa Uganda, wateja wengi zaidi wa benki hizo sio waislamu.
''Ukienda kwenye huduma za Benki ya Kiislamu mkikubaliana na benki kuwa faida itakuwa ni asili mia kadhaa, haibadiliki kamwe, hata baada ya miaka mitano, miaka kumi au miaka ishirini,'' aeleza Issa.
Wengi wakisikia hivyo wanauliza basi benki zinapata vipi faida?
Faida zinatoka pale benki zinapofanya hesabu ya kutoza hizo faida zake kwa wateja, zinazingatia mabadiliko yatakayotokea katika mambo ya fedha nchini, kama thamani ya fedha na mengine.
Umaarufu wa huduma hizi za benki za Kiislamu umesambaa kwa nchi nyingi nje ya zile za asili ya kiislamu. Issa anasema kuwa Mataifa kaskazini mwa Jangwa la Sahara karibu zote zimekuwa zikitumia mfumo huu wa Benki.
Nigeria, Senegal, Mali, Gambia na Niger pia zimejikita katika mfumo huu. Kusini mwa Jangwa la Sahara, Sudan ndio ilitangulia.
Lakini sasa ndio Afrika Mashariki imechangamkia ukianza na Kenya, tangu mwaka 2005, Ikafuatia Tanzania, Burundi, Rwanda na sasa Uganda inajiunga. Na hivi karibuni nchi kama Zambia na Zimbabwe zimeonesha nia na huenda nchi zaidi zitajiunga hivi karibuni.
Hii inatokana na kuingia kwa hati fungani za Kiislamu (Islamic Bonds), ambazo ndizo zinalazimisha kuwepo huduma fulani za kifedha za Kiislamu ili zitekelezeke.
Japo Islamic Banking inaonekana kusambaa kwa haraka, bado iko mbali sana. Wataalamu wanasema kuwa mfumo huu wa kifedha wa Kiislamu ni takriban 1.2% ya mfumo wote wa fedha wa dunia.
Hata hivyo changa moto kubwa ni namna ya utekelezaji wa huduma hizi katika mataifa ambayo sio ya Kiislamu. Kanuni za mfumo wa kifedha za Kiislamu zinagongana na kanuni za mfumo wa fedha zisizokuwa za Kiislamu.
''Kutokana na hilo, panahitaji kwanza mabadiliko makubwa ya mabadiliko ya sera za fedha na mabadiliko ya kanuni za fedha na hata sheria za kodi ili zifanye huduma hizi ziweze kutumika,'' anasema Mohammed Issa.
Kuambatana na mtazamo huu, hatua ya Uganda ya kufanyia mabadiliko sheria ya kifedha ya Uganda itaondoa vikwazo vilivyokuwepo ili kuiwezesha Uganda kutekeleza huduma hizi.