Mamlaka ya wanyamapori nchini Zimbabwe imetetea mpango wake wa kuwauwa tembo 200 ili kupunguza shinikizo kwa rasilimali zinazokabiliwa na ukame baada ya kukosolewa.
Ilipotangazwa wiki iliyopita, mamlaka hiyo ilisema kuwa hatua ya kwanza ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka 35 ilikuwa muhimu kwani Zimbabwe ilikuwa ikijitahidi kukabiliana na wingi wa wanyama hao wakubwa pamoja na ukame ambao umewaacha maelfu bila chakula.
Uamuzi wa Zimbabwe ulikuja baada ya nchi jirani ya Namibia kusema inapanga kuwaua zaidi ya wanyamapori 700, ikiwa ni pamoja na tembo 83, ili kupunguza shinikizo kwenye malisho yake yaliyoathiriwa na ukame na usambazaji wa maji, na kutoa nyama kwa ajili ya mpango wa msaada wa chakula.
Kukabiliana na ukosoaji
Maamuzi ya Zimbabwe na Namibia yamekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa wahifadhi na vikundi vya haki za wanyama.
Lakini kutokana na kuwa na idadi kubwa ya tembo nchini Zimbabwe inayokadiriwa kufikia 84,000, hatari itakuwa kidogo sana, msemaji wa Mamlaka ya Mbuga na Wanyamapori ya Zimbabwe (ZimParks) Tinashe Farawo aliiambia AFP.
ZimParks hapo awali ilikadiria kuwa karibu tembo 100,000 nchini humo.
"Ukifanya hesabu ya watakaouawa kwa chakula utaona ni kidogo sana, watu hawataki kuona umuhimu wake."
Sambaza nyama
Nyama yao itasambazwa kwa watu wanaohitaji msaada wa chakula na pembe hizo zitawekwa kwa hifadhi ya tani 130 za pembe za ndovu, msemaji huyo alisema.
Hatua ya kuwawinda tembo hao kwa ajili ya chakula ilikosolewa na baadhi ya watu, skwa sababu wanyama hao ni kivutio kikubwa kwa watalii.
"Serikali lazima iwe na mbinu endelevu zaidi za kiikolojia za kukabiliana na ukame bila kuathiri utalii," alisema Farai Maguwu, Mkurugenzi wa Kituo kisicho cha faida cha Utawala wa Maliasili. "Wanahatarisha kuwafukuza watalii kwa misingi ya kimaadili. Tembo wana faida kubwa kuwa hai kuliko kufa," Maguwu aliongeza.
Kupambana na idadi kubwa ya tembo
Ikiwa inakadiriwa kuwa na tembo wa pili kwa ukubwa duniani baada ya Botswana, Farawo alisema Zimbabwe "inapambana na idadi kubwa ya tembo."
"Wanaangusha miti, wanaharibu kila kitu, kwa sababu idadi si endelevu. Mfumo wetu wa ikolojia hauwezi kuendeleza kile tulichonacho sasa," alisema.
Farawo aliongeza kuwa ukame ulikuwa unawapeleka tembo na wanyamapori wengine katika makazi ya watu kutafuta chakula na maji, matukio ambayo wakati mwingine huwa hatari.
"Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, watu 30 waliuawa katika makabiliano katika wanyamapori, huku tembo wakichangia asilimia 60 ya vifo," alisema.
Mnamo 2023, ZimParks ilipokea simu 3,000 za malalamiko zinazohusiana na wanyama pori.
Uhifadhi wa gharama kubwa
Farawo alisema kuwa uhifadhi ni ghali na hatua za ulinzi wa wanyamapori nchini Zimbabwe kama vile doria za kupambana na ujangili zinagharimu dola milioni 6 hadi 7, ambazo inabidi kuzisaka kutoka kwa washirika mbalimbali.
Nchi hiyo kwa wakati huo haiwezi kuuza akiba yake ya pembe kutokana na marufuku ya kimataifa ya biashara ya pembe za ndovu.
Pia haina njia ya kusambaza tembo kwenye sehemu zenye msongamano mdogo wa nchi, ikiwa mara ya mwisho ilifanya hivyo ilikuwa 2019.
Namibia na Zimbabwe ni miongoni mwa nchi nyingi kusini mwa Afrika ambazo zimetangaza hali ya hatari kutokana na ukame.