Hesabu ya awali iliyotolewa na shirika la habari la ZBC Ijumaa jioni, ZANU-PF iliongoza kwa viti vya ubunge, 125 kati ya 210 huku Chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kikijizolea viti 59. / Picha :  X - Jumuiya ya Madola 

Waangalizi wa kigeni wa uchaguzi wamesema kuwa uchaguzi wa urais na wabunge wa Zimbabwe umeshindwa kuenda sambamba na viwango vya kikanda na kimataifa, na kutilia shaka uaminifu wa kura hiyo yenye mvutano.

Waangalizi wa kikanda na kimataifa wametaja wasiwasi juu ya kupigwa marufuku kwa mikutano ya upinzani, kunyimwa kibali kwa vyombo vya habari kadhaa vya kigeni, kukosa majina ya wapiga kura kwenye orodha katika vituo vyao vya kupigia kura, vyombo vya habari vya serikali vilivyoegemea upande mmoja na vitisho kwa wapiga kura miongoni, mwa masuala yaliyovuruga uchaguzi.

Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Fabio Massimo Castaldo, alisema siku ya Ijumaa uchaguzi "ulipungukiwa na viwango vingi vya kikanda na kimataifa".

"Vurugu na vitisho hatimaye vilizua hali ya hofu," alisema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola Amina Mohamed, kutoka Kenya alisema mchakato wa kupiga kura "uliendeshwa vyema na wa amani," kwa ujumla, lakini "baadhi ya masuala muhimu" yaliathiri "uaminifu" na "uwazi" wa uchaguzi.

"Baadhi ya vipengele vya uchaguzi havikufikia matakwa ya katiba ya Zimbabwe, sheria ya uchaguzi na kanuni na miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia," alisema mkuu wa ujumbe wa kambi ya kikanda Nevers Mumba, makamu wa rais wa zamani wa Zambia.

Hilo lilikuwa ni karipio nadra kutoka kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yenye mataifa 16, huku kwa kawaida, waangalizi wake huidhinisha uchaguzi katika nchi wanachama.

Hata hivyo, Chama tawala cha ZANU-PF kilijitetea kwa hasira, na kutupilia mbali mitazamo kutoka nchi za Magharibi kama "mawazo ya kikoloni" yanayotoka kwa mataifa ya zamani ya kikoloni yasiyokuwa na haki ya kuifundisha Zimbabwe demokrasia.

"Tunatupilia mbali minong'ono, midomo ya Nevers Mumba," msemaji wa chama Christopher Mutsvangwa aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Harare, akimwelezea mkuu wa ujumbe wa SADC kama "mhubiri" mwenye upendeleo.

"Hatuwezi kuwa wakamilifu. Lakini kwa hakika hakuna nia mbaya katika kutokamilika kwetu," alisema kuhusu mchakato wa kupiga kura.

Mapungufu ya kimsingi

Uchaguzi huo unafuatiliwa kwa karibu kote kusini mwa Afrika kama kipimo cha uungwaji mkono kwa Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80 wa ZANU-PF, chama ambacho utawala wake wa miaka 43 umekumbwa na uchumi unaodorora na tuhuma za udikteta.

Upigaji kura ulilazimika kuendelea hadi siku ya pili isiyotarajiwa kutokana na kucheleweshwa kwa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura katika baadhi ya wilaya muhimu, ikiwemo ngome ya upinzani mjini Harare.

Kwa mujibu wa hesabu ya awali iliyoonyeshwa na shirika la habari la ZBC Ijumaa jioni, ZANU-PF iliongoza katika kinyang'anyiro cha ubunge, baada ya kujinyakulia viti 125 kati ya 210 huku Chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kikijizolea viti 59.

Viti vingine 60 huteuliwa kupitia mfumo wa orodha ya vyama vya uwakilishi sawia.

Chama cha upinzani CCC, kilichozuiwa kufanya zaidi ya mikutano 100 yake ya kampeni kupitia marufuku, ilikemea mchakato wa uchaguzi kuwa "wenye dosari za kimsingi". Chini ya robo ya vituo vya kupigia kura mjini Harare, ngome ya upinzani, ndivyo vilifunguliwa kwa wakati Jumatano, siku ya kwanza ya upigaji kura.

Chagamoto hizo zilimlazimu Mnangagwa, anayewania muhula wa pili, kutoa agizo la usiku wa manane wa kuongeza muda wa kura kwa siku moja zaidi.

Tume ya uchaguzi ilisema ina uhakika wa kutangaza matokeo ya mwisho kabla ya tarehe ya mwisho ya Jumanne.

'Wasiwasi mkubwa'

Kiongozi wa CCC Nelson Chamisa alikashifu ucheleweshaji huo kama "kesi ya wazi ya kukandamiza wapiga kura, kesi ya kawaida ya wizi wa enzi za kale "Stone Age".

Chamisa, mwenye umri wa miaka 45, ndiye mpinzani mkuu wa Mnangagwa, 80, ambaye aliingia madarakani baada ya mapinduzi yaliyomwondoa madarakani kiongozi marehemu Robert Mugabe mnamo 2017.

Chamisa, mwenye umri wa miaka 45, ndiye mpinzani mkuu wa Mnangagwa, 80, ambaye aliingia madarakani baada ya mapinduzi yaliyomwondoa madarakani marehemu mtawala Robert Mugabe mnamo 2017.

Wakati huo huo, waangalizi 41 wa ndani walikamatwa usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi na kupokonywa kompyuta na simu zao za mkononi na polisi ambao walidai vifaa hivyo "vilitumika kujumlisha" matokeo ya vituo vya kupigia kura kinyume cha sheria, wakielezea shughuli hiyo kama "ukatili na uhalifu".

Wengi wa watu hao waliokamatwa, hasa wanawake na wanaume kati ya umri wa miaka 20 na 30, wanaofanya kazi na asasi za kiraria zinazounga mkono demokrasia, walifika Ijumaa katika mahakama ya Harare wakiwa wamebanana nyuma ya lori nyeupe kujibu mashtaka yaliyowakabili.

"Polisi waliokuwa wamejihami kwa bunduki aina ya AK-47, na aina nyingine ya silaha waliwavamia washtakiwa na kuwakamata kwa mtindo wa kukokotwa," wakili wa upande wa utetezi Alec Muchadehama alimweleza hakimu, ambaye alitoa dhamana ya $200.

Kukamatwa huko kunazidisha "wasiwasi wetu," alisema mkuu wa waangalizi wa uchaguzi wa EU.

"Kufikia sasa, yote yanaashiria uchaguzi wenye utata," alisema Kealeboga Maphunye, profesa wa masomo wa Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, katika mdahalo wa mtandaoni ulioandaliwa Ijumaa na Ofisi ya Uhusiano ya Kusini mwa Afrika yenye makao yake makuu Afrika Kusini.

AFP