Hatua hii ni mara ya kwanza kufanyika nchini tangu 1988 litafanyika katika wilaya za Hwange, Mbire, Tsholotsho na Chiredzi/ Picha: AP

Zimbabwe inapanga kuwaua tembo 200 ili kulisha jamii zinazokabiliwa na njaa kali baada ya ukame mbaya kuwahi kutokea katika miongo minne, mamlaka ya wanyamapori ilisema Jumanne.

"Tunaweza kuthibitisha kwamba tunapanga kuwaua takriban tembo 200 kote nchini. Tunashughulikia mbinu za jinsi tutakavyofanya," Tinashe Farawo, msemaji wa Mamlaka ya Hifadhi na Wanyamapori ya Zimbabwe (Zimparks) aliiambia Reuters.

Alisema nyama ya tembo itagawiwa kwa jamii nchini Zimbabwe zilizoathiriwa na ukame.

Hatua hiyo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika nchini tangu mwaka 1988, itafanyika katika wilaya za Hwange, Mbire, Tsholotsho na Chiredzi. Inafuatia uamuzi wa nchi jirani ya Namibia mwezi uliopita wa kuwaua ndovu 83 na kusambaza nyama kwa watu walioathiriwa na ukame.

Zaidi ya tembo 200,000 wanakadiriwa kuishi katika eneo la hifadhi lililoenea katika nchi tano za kusini mwa Afrika - Zimbabwe, Zambia, Botswana, Angola na Namibia - na kufanya eneo hilo kuwa moja ya idadi kubwa ya tembo duniani kote.

Farawo alisema mauaji hayo pia ni sehemu ya juhudi za nchi kupunguza msongamano wa tembo katika mbuga zake, ambazo zinaweza kuhimili tembo 55,000 pekee. Zimbabwe ina zaidi ya tembo 84,000.

"Ni jitihada za kupunguza msongamano wa hifadhi katika mazingira ya ukame, idadi ni tone tu katika bahari kwa sababu tunazungumzia 200 (tembo) na tunakaa pamoja na 84,000, ambayo ni kubwa," alisema.

Kwa ukame huo mkubwa, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori inaweza kuongezeka huku rasilimali ikizidi kuwa chache. Mwaka jana Zimbabwe ilipoteza watu 50 kutokana na mashambulizi ya tembo.

Nchi hiyo, ambayo inasifiwa kwa juhudi zake za uhifadhi na kuongeza idadi ya tembo, imekuwa ikishinikiza kongamano la Mataifa wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) ili kufungua tena biashara ya meno ya tembo na tembo hai.

Ikiwa na mojawapo ya idadi kubwa ya tembo, Zimbabwe ina takriban dola 600,000 za akiba ya pembe za ndovu ambazo haiwezi kuziuza.

TRT Afrika na mashirika ya habari