Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris akizungumza na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan - Ikulu

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ameondoka Tanzania baada ya ziara ya siku tatu ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Afrika. Aliwasili juzi kwa ajili ya mkutano wake na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

"Ziara yake ililenga kupunguza kasi ya ushawishi wa China na washirika wake katika ukanda huu," anasema Jawadu Mohamed, mchambuzi wa kisiasa kutoka Tanzania.

Makamu wa Rais pia amezungumza na asasi za kiraia, wakiwemo viongozi vijana, wawakilishi wa wafanyabiashara, wajasiriamali na wenyeji wa Afrika waishio ughaibuni.

Ziara hiyo imefanyika miezi michache baada ya Mkutano wa hivi karibuni wa Viongozi wa Marekani na Afrika ulioandaliwa na Rais Joe Biden jijini Washington Desemba 2022.

Madhumuni ya Ziara

Ikulu ya White House imetangaza kuwa ziara hii itaimarisha ushirikiano wa Marekani na bara zima la Afrika na kuendeleza jitihada za pamoja za usalama na ustawi wa kiuchumi.

Makamu wa Rais, Harris atashirikiana na Serikali za Afrika na sekta ya binafsi kupanua fursa za uchumi wa kidijitali, kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kupitia uvumbuzi, ujasiriamali, na uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake.

"Makamu wa Rais pia anajaribu kuweka msisitizo wa utamaduni wa Marekani ambao wanahisi umepotea kutokana na baadhi ya mila zao kutofungamana na za Tanzania," Mohamed aieleza TRT Afrika,

Akiongeza. "Marekani haipo tu kwa kile wanachouza, lakini inahisi wako hapa, kama ilivyo jitokeza hivi karibuni, pia kutetea ajenda ya mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ) na itajaribu kukazia kipengele cha haki za binadamu nyuma ya ajenda hio."

Ingawa ziara ya Makamu wa Rais Harris ni hatua chanya, ni muhimu kutambua historia tata ya ushirikiano kati ya Marekani na Afrika. Marekani ina historia ndefu ya kunyonya rasilimali za Kiafrika na kuunga mkono tawala za kimabavu, mchambuzi huyo wa siasa anafafanua.

Anasisitiza kuwa, Marekani imekuwa ikishiriki katika kuvuruga utulivu wa nchi kadhaa za Afrika, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa makundi yenye itikadi kali katika eneo hilo.

Makamu wa Rais amemaliza ziara yake nchini Ghana, ambapo alikutana na Rais Nana Akufo-Addo kujadili vitisho vya usalama vinavyoletwa na makundi yenye itikadi kali katika eneo la Sahel.

Pia saa chache zilizo pita amekamilisha ziara yake nchini Tanzania.

Mkazo kwa Kampuni Changa

Katika ziara hii, eneo maalum ambalo limeonekana kuvutia nia ya Marekani ni katika uwekezaji kwa kampuni changa na wajasiliamli wabunifu katika nchi hio. Tanzania inashika nafasi ya nane katika ukanda wa Afrika, huku dola milioni 11 zikipelekwa katika miradi 11 tofauti.

"Ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani nchini, na dhamira yake ya kuvuta wawekezaji na ushawishi wake una nguvu ya kubadisha fikra za wafanyabiashara, hasahasa kama wito unatoka kwa kwa Makamu wa Rais mwenyewe." anafafanua Mmiliki na Mwanzilishi wa jukwaa la kujifunza kidigitali la Mtabe, Given Edward.

"Kitendo chake cha kutilia maanani katika eneo la ubunifu kunatoa picha kwa ulimwengu kuwa kuna jambo kubwa linaendelea hapa. Hatupaswi kuiona kama ziara ya kawaida; ikiwa tunaweza kupata ahadi kutoka kwake na timu yake, hilo tu linatosha kusaidia katika kuvutia uwekezaji hata baada ya kuondoka”. Edward aliongeza.

Ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Harris nchini Tanzania ni fursa kwa Marekani kuimarisha ushirikiano wake na nchi za Afrika na kuendeleza juhudi za pamoja za usalama na ustawi wa kiuchumi.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua historia changamano ya ushirikiano wa Marekani na Afrika na kuhakikisha kwamba mkakati wa Marekani unaongozwa na tafakari ya kina kuhusu jinsi wanavyokuza demokrasia na haki za binadamu.

TRT Afrika na mashirika ya habari