Mlipuko wa kipindupindu nchini Zambia umesababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na kuambukiza 10,000.
Ugonjwa huo umegunduliwa katika karibu nusu ya wilaya za nchi na mikoa tisa kati ya 10, na taifa la watu wapatao milioni 20 limekuwa likirekodi zaidi ya kesi 400 kwa siku.
Mpaka Jumapili ya tarehe 21, Januari, mwaka huu takwimu kutoka kitengo cha taifa afya cha Zambia zinaonyesha kuwa tangu kutokea mlipuko wa ugonjwa huo, Oktoba 2023, kumekuwa na jumla ya visa 12, 338 hadi sasa.
Kati ya hivyo, wale ambao bado wamelazwa katika hospitali ni 847, huku wengine wakiruhusiwa kwenda nyumbani.
Kati ya idadi hiyo walioaga dunia kutokana na ugonjwa huo mpaka sasa wamefikia 480.
Ezra Banda wa Shirika linaloitwa Keepers Zambia, ambaye anasaidia katika kutoa usaidizi kwa wagonjwa anasema, "Changamoto iliyo na Wazambia wengi sasa ni pengo la taarifa juu ya jinsi gani wanaweza kuzuia kuambukizwa kipindupindu na hii inazidishwa na ukosefu wa maji safi na salama lakini pia vifaa vya vyoo."
Uzito wa maambukizi hayo umeifanya serikali kutoa agizo la kufunga zote shule nchini baada ya likizo za mwisho wa mwaka.
Serikali ya Zambia imeanzisha mpango wa chanjo kwa wingi na inasema inatoa maji safi - lita milioni 2.4 kwa siku - kwa jamii ambazo zimeathirika katika taifa zima la kusini mwa Afrika.
Uwanja mkubwa wa soka katika mji mkuu wa Lusaka umebadilishwa kuwa kituo cha matibabu.
Mlipuko wa kipindupindu, ulioripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2023, umeongezeka tangu katikati ya mwezi Disemba mwaka jana.
"Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wameunga mkono mwitikio unaoongozwa na serikali, wakitoa zaidi ya Chanjo za Kipindupindu milioni 1.4," Shirika la UNOCHA la Afrika Kusini na Afrika Mashariki limesema.
"Chanjo milioni 1.4 zinazotumika sasa zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO, ni nyongeza inayokaribishwa kwa kupambana na kipindupindu. Ugonjwa huu bado unaendelea, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuzingatia miongozo ya afya," rais wa Zambia Hakainde Hichilema amesema katika akaunti yake ya X.