Zambia, ambayo ilitangaza ukame kama janga la kitaifa mwezi Februari, imebakiwa na dola milioni 51 tu kati ya dola milioni 940 zinazohitaji kukabiliana na janga hilo.
Zambia ilisema inahitaji karibu dola bilioni moja kukabiliana na ukame mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa na nchi hiyo na kutoa msaada wa "kuokoa maisha" ya mamilioni ya watu.
Siku ya Jumanne, kupitia hotuba yake kwa njia ya televisheni, Hichilema amesema kuwa takriban nusu ya watu milioni 20 wa taifa hilo la kusini mwa Afrika wameathiriwa vibaya na kiangazi cha muda mrefu kinachosababishwa na hali ya hewa ya El Nino.
"Zambia imepata mvua ya kiwango cha chini mno mwaka huu, na hivyo kupelekea ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini," alisema.
Ukosefu wa mvua umeathiri sekta ya kilimo, na kuathiri mazao na malisho, Hichilema alisema.
Msaada wa haraka
Zaidi ya watu milioni 6 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu nchini humo.
Lakini Zambia, ambayo ilitangaza ukame kuwa janga la kitaifa mwezi Februari, ina takriban dola milioni 51 tu kati ya dola milioni 940 inazohitaji kukabiliana na tatizo hilo, aliongeza.
"Kwa moyo mzito, kwa niaba ya serikali yetu na watu wa Zambia, tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, washirika wetu ndani ya nchi, sekta binafsi, kanisa na mashirika ya kiraia, kuunga mkono mpango wetu wa kifedha na mali. Kupunguza athari mbaya za ukame," alisema.
Joto duniani
Mwenendo wa asili ya hali ya hewa ya El Nino, ambayo iliibuka katikati ya 2023, kwa kawaida huongeza viwango vya joto duniani kwa mwaka mmoja baadaye.
Kwa sasa inaleta maafa katika eneo la kusini mwa Afrika, ambapo Zimbabwe na Malawi pia zimetangaza janga la kitaifa na kuomba msaada wa kimataifa kutokana na ukosefu wa mvua.