Zaidi ya watu 80 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamefariki baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama, Rais Felix Tshisekedi ametangaza.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano kwenye Mto Kwa, takriban kilomita 70 (maili 43) kutoka jiji la Mushie katika jimbo la Mai-Ndombe.
"Rais wa Jamhuri anatoa wito wa kufanyika uchunguzi wa sababu za kweli za tukio hili la kusikitisha, ili kuzuia janga kama hili kutokea tena siku zijazo," urais ulisema katika taarifa iliyoandikwa kwenye X.
Tshisekedi "anatuma rambirambi zake kwa familia na wapendwa wa waathirika," taarifa hiyo ilisema, ikiongeza kuwa aliwaelekeza mamlaka kuchukua hatua na kuwasaidia wale walioathirika.
Ajali hiyo ni kutokana na na safari ya usiku, alisema gavana wa jimbo la Mai-Ndombe, Rita Bola Dula, akiiambia shirika la habari la Reuters, na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea.
Ajali za boti zinazosababisha vifo ni za kawaida DRC, ambapo vyombo vya usafiri mara nyingi hujazwa zaidi ya uwezo wao. Nchi hiyo ya Afrika ya Kati ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri wa mtoni ni wa kawaida.