WHO yatafakari iwapo itatangaza dharura ya Mpox

WHO yatafakari iwapo itatangaza dharura ya Mpox

Kwa sasa nchi 12 barani Afrika zimetangaza kuwa na wagonjwa wa Mpox
Nchi 12 barani Afrika zimetangaza kuwa na kesi ya Mpox/ Picha: Wengine

Shirika la Afya Duniani, World Health Organisation, WHO, limesema kuwa litaamua ikiwapo kuna haja ya kutangaza dharura ya afya kutokana na maambukizi ya Mpox.

"Ninafikiria kuitisha Kamati ya dharura ya kanuni za afya ya kimataifa ili kunishauri kama mlipuko wa Mpox unapaswa kutangazwa kuwa dharura ya afya ya umma," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom alisema katika akaunti yake ya X.

Kwa sasa nchi 12 barani Afrika zimetangaza kuwa na wagonjwa wa Mpox.

"Huku aina mbaya zaidi ya Mpox inavyoenea katika nchi nyingi za Kiafrika, WHO na Shirika ya Afya la Umoja wa Afrika, Africa CDC, serikali za mitaa na washirika wanaongeza zaidi mwitikio wa kuzuia maambukizi ya magonjwa. Lakini ufadhili zaidi na msaada kwa ajili ya majibu ya kina unahitajika," Adhanom aliongezea.

Maambukizi hayo yameripotiwa katika nchi 12 za Afrika zikiwemo Kenya na Burundi.

Jamhuri ya Kidemokrais ya Congo, DRC, ina zaidi ya 96% ya kesi zote na vifo.

Maafisa walisema karibu 70% ya kesi nchini DRC ni za watoto chini ya miaka 15, ambao pia walichangia 85% ya vifo.

Kumekuwa na kesi 14, 250 zinazokadiriwa kufikia sasa, nyingi zikiwa za mwaka jana.

Ikilinganishwa na miezi saba ya kwanza ya 2023, CDC ya Afrika ilisema kesi zimeongezeka kwa 160% na vifo vimeongezeka 19%, hadi 456.

TRT Afrika