Israel imetangaza kuwa inapanga uvamizi wa ardhini Gaza na wakaazi wa eneo ilo wameanza kukimbia / Picha: AP

Maelfu ya Wapalestina wanatoroka kutoka kaskazini mwa Gaza baada ya jeshi la Israel kuamuru takriban watu milioni moja kuondoka.

Israel imetangaza kuwa inapanga uvamizi wa ardhini kufuatia shambulio la kushtukiza wiki moja iliyopita na kundi la walipaganji wa Hamas.

Shirika la Afya Duniani, WHO, inajiunga na mashirika mengine ya kimataifa katika kuiomba Israel kubatilisha mara moja maagizo ya kuwahamisha zaidi ya watu milioni moja wanaoishi kaskazini mwa eneo la Gaza.

"Tunaendelea na ombi letu kwa Israeli kufikiria upya uamuzi wa kuwahamisha watu milioni 1.1. Itakuwa janga la kibinadamu'' shirika la WHO limesema katika taarifa.

"Uhamisho wa watu wengi utakuwa mbaya kwa wagonjwa, wafanyakazi wa afya na raia wengine walioachwa nyuma au waliopatikana katika harakati za watu wengi," imeongezea taarifa hiyo.

Hospitali mbili za Wizara ya Afya Kaskazini mwa Gaza zinaendelea kufanya kazi huku wagonjwa wakiwa wengi kuliko uwezo wao/ Picha: AA

Wataalam wa afya wanasema huku mashambulizi ya anga yanayoendelea na mipaka imefungwa, raia hawana mahali salama pa kwenda. "

Takriban nusu ya wakazi wa Gaza wanaripotiwa kuwa umri wa chini ya miaka 18.

"Kwa kupungua kwa usambazaji wa chakula salama, maji safi, huduma za afya, na bila makazi ya kutosha, watoto na watu wazima, pamoja na wazee, wote watakuwa katika hatari kubwa ya magonjwa," WHO imesema.

Wizara ya Afya ya Palestina imefahamisha WHO kwamba kuwahamisha wagonjwa walio hospitalini kwa hali ya hatari haiwezekani bila kuhatarisha maisha yao.

Wagonjwa walio katika mazingira magumu ni pamoja na wale ambao wamejeruhiwa vibaya au wanaotegemea msaada wa maisha. Kuwahamisha huku kukiwa na uhasama kunaweka maisha yao hatarini mara moja.

Hospitali mbili za Wizara ya Afya Kaskazini mwa Gaza ambazo zinaendelea kufanya kazi, zimeripoti kuwa zimepitisha uwezo wao wa vitanda 760 kwasababu ya msongamano mkubwa wa wagonjwa na waliojeruhiwa.

TRT Afrika