Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiorodhesha Cabo Verde miongoni mwa nchi zisizo na malaria, na hivyo kuashiria mafanikio makubwa katika afya duniani.
Kutokana na tangazo hilo, Cabo Verde inajiunga katika orodha ya nchi 43 na eneo 1 ambalo WHO imetoa cheti hiki.
"Ninaipongeza serikali na watu wa Cabo Verde kwa kujitolea kwao bila kuyumbayumba na ustahimilivu katika safari yao ya kutokomeza malaria," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema.
Uthibitisho wa kutokomeza malaria ni utambulisho rasmi wa WHO wa hali ya nchi kutokuwa na malaria.
Unatolewa wakati nchi imeonyesha - kwa ushahidi mkali na wa kuaminika - kwamba maambukizi ya malaria ya kienyeji na mbu aina ya Anopheles umekatizwa nchini kote kwa angalau miaka mitatu mfululizo iliyopita.
Nchi lazima pia ionyeshe uwezo wa kuzuia maambukizi mapya.
"Mafanikio ya Cabo Verde ni ya hivi punde zaidi katika mapambano ya kimataifa dhidi ya malaria, na yanatupa matumaini kwamba kwa kutumia zana zilizopo, pamoja na mpya ikiwa ni pamoja na chanjo, tunaweza kuthubutu kuwa na ndoto ya ulimwengu usio na malaria," Tedros ameongezea.
Cabo Verde ni nchi ya tatu kuthibitishwa katika kanda ya Afrika na WHO, ikiungana na Mauritius na Algeria ambazo ziliidhinishwa mwaka wa 1973 na 2019.
"Udhibitisho wa nchi kutokuwa na malaria una athari kubwa, na imechukua muda mrefu kufikia hatua hii. Kwa upande wa picha ya nje ya nchi, hii ni nzuri sana, kwa utalii na kwa kila mtu mwingine. Changamoto ambayo Cabo Verde imeshinda katika mfumo wa afya inatambulika,” alisema Waziri Mkuu wa Cabo Verde, Ulisses Correia e Silva.
Changamoto ya Malaria ndio kubwa zaidi katika bara la Afrika, ambalo lilichangia takriban asilimia 95 ya visa vya malaria duniani na asilimia 96 ya vifo vinavyohusiana, kulingana na takwimu za 2021.
Utalii unachukua takriban asilimia 25 ya pato la taifa la Cabo Verde.
WHO inasema kuwa mifumo na miundo iliyojengwa kwa ajili ya kutokomeza malaria imeimarisha mfumo wa afya na itatumika kupambana na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu kama vile homa ya dengue.
Wasafiri kutoka maeneo yasiyo na malaria sasa wanaweza kusafiri hadi visiwa vya Cabo Verde bila hofu ya maambukizi ya malaria ndani na uwezekano wa usumbufu wa hatua za kuzuia matibabu.
Cabo Verde, kisiwa chenye visiwa 10 katika Bahari ya Atlantiki ya Kati, kimekabiliwa na changamoto kubwa ya malaria.
Kabla ya miaka ya 1950, visiwa vyote viliathiriwa na malaria.
Milipuko mikali ilikuwa ikitokea mara kwa mara katika maeneo yenye watu wengi zaidi hadi hatua zilizolengwa zilipotekelezwa. Kupitia matumizi yaliyolengwa ya kunyunyizia dawa, nchi iliondoa malaria mara mbili: mwaka 1967 na 1983.