Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelaani uvamizi uliofanywa kwenye maghala yake jijini Bukavu, kusini mwa jimbo la Kivu, huku kukiwa na hofu ya usalama katika eneo la Mashariki mwa DRC.
“Vyakula hivyo muhimu vilihifadhiwa kwa ajili ya familia ambazo ziko katika wakati mgumu kwa sasa,” lilisema Shirika hilo kupitia ukurasa wake wa X.
Aidha, WFP imeongeza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula na usambazaji wake inazidi kuwa ngumu kutokana na kuongezeka kwa machafuko katika eneo hilo.
“Tunaziomba pande zinazohasimiana kumaliza mgogoro huo na kuheshimu mikataba ya kimataifa yenye kulinda raia na watu wengine,” taarifa hiyo ilisema.
Tukio hilo limetokea baada ya waasi wa M23 ambao wanapambana na vikosi vya serikali kudai kuwa wanashikilia uwanja wa ndege wa Kavumu, ulioko kilomita 25 kutoka mji mkuu wa Bukavu.