Baadhi ya wavuvi waliookolewa nchini Kenya baada ya kupotea kwa siku 22. Picha/ TRT Afrika. 

Na Diana Wanyonyi

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Wavuvi watatu nchini Kenya waliotoweka kwa siku 22 huko Malindi katika Bahari ya Hindi hatimae wamerudishwa makwao huku kukiwa na hofu ya mmoja wao kupoteza maisha. Taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha wavuvi hao kupotea ni baada ya injini yao ya boti kuharibika kwa kupigwa na mawimbi makali.

Wavuvi hao ni Hanseey Baraka Kilian, Akida Idd Mohamed na Fahad Ali Mohamed waliokolewa baharini na meli ya uvivu ya Uchina baada ya kutoweka tarehe 30 mwezi Novemba mwaka huu.

Wavuvi hao walipokelewa katika pwani ya Liwatoni kisiwani Mombasa na Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini nchini humo Salim Mvurya, baada ya mabaharia hao kuwasili bandarini kwa chombo cha Maafisa wa Huduma za Usalama Baharini-Kenya Coast Guard Service.

Wavuvi hao walipokelewa katika pwani ya Liwatoni kisiwani Mombasa na Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini nchini humo Salim Mvurya. Picha/TRT Afrika.

Wavuvi hao waliokuwa wamevalia ovaroli nyekundu huku miguuni wamevaa viatu vya plastiki walionekana wamedhoofika, huku wakiwa katika msongo ya mawazo.

Familia, ndugu na jamaa za wavuvi hao walifika bandarini wakitarajia kuungana na wapendwa wao ila wavuvi hao waliwahishwa hospitali ya Mombasa kwa ajili ya kupata matibabu na kupokea ushauri nasaha.

“Nilikuwa kwenye hali ngumu. Sina nguvu kabisa, familia yetu yote yaani kila mmoja alikuwa katika njia panda akisubiri kujua hatma ya wao.” alisema Lilian.

Waziri Mvurya aliwapongeza maafisa wa huduma za usalama baharini kwa uokoaji huku akiwashukuru wavuvi wa taifa la Uchina waliowaokoa watatu hao.

“Nachukua nafasi hii kuwatangazia Wakenya kwamba wale wavuvi ambao walikuwa wamepotea siku 22 zilizopita, tumeweza kuwapokea watatu wakiwa salama na yule mmoja bado anatafutwa. Napongeza juhudi ya vikosi vyetu vya usalama wa baharini na wadau wote walioshiriki katika jambo hili,” amesema Mvurya.

Waziri huyo ameongeza kusema, “Nataka kusema kuwa kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi (climate change) kuna mabadiliko makubwa sana, upepo na mawimbi pia yamebadilika. Nataka kuchukua fursa hii kuwafahamisha washikadau katika sekta ya uvuvi maeneo ya baharini, maziwa na mito kuwa makini ili kuhakikisha vyombo vya uvuvi havitelezi na kuondoka ufukweni.”

Mkurugenzi Mkuu wa Maafisa wa Huduma za Usalama Baharini Bruno Shioso amesema wamejitolea kuhakikisha kwamba wanaendesha kikosi cha kisasa zaidi na wataangalia uwezo ulioimarishwa katika shughuli za utafutaji na uokoaji.

Alisema kuwa kila mwaka, wanashughulikia zaidi ya kesi 900 sawa na hizo zinazohusu utafutaji na uokoaji nchini kote huku asilimia 62 ya kesi hizo zikiwa Pwani.

TRT Afrika