Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu, idadi ya awali ya watu waliouawa imefika 104 katika vijiji 18 katika eneo la Bokkos. Picha: Reuters

Idadi hii mpya ya vifo iliyotangazwa inaashiria ongezeko la kasi la idadi ya waliouawa tofauti na takwimu za awali ya watu 16 iliyoripotiwa na jeshi Jumapili jioni katika eneo lililokumbwa na mvutano wa kidini na kikabila kwa miaka kadhaa.

"Watu 113 wamethibitishwa kuuawa katika uhasama wa Jumamosi ulioendelea hadi saa za mapema za Jumatatu," Kassah, mkuu wa serikali ya eneo hilo la Bokkos, Jimbo la Plateau, aliiambia AFP.

Magenge yenye silaha, yanayojulikana kama "majambazi," yalianzisha mashambulizi "yaliyopangwa" dhidi ya "jamii tofauti zisizopungua 20" na kuchoma moto nyumba, Kassah alisema.

"Tulipata zaidi ya watu 300 waliojeruhiwa" ambao wamefikishwa hospitali huko Bokkos, Jos na Barkin Ladi, alisema.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu, idadi ya awali ya watu waliouawa imefika 104 katika vijiji 18 katika eneo la Bokkos.

Takriban watu 50 pia wameripotiwa kufa katika vijiji kadhaa vilivyopo eneo la Barkin Ladi, kulingana na Dickson Chollom, mwanachama wa bunge la jimbo.

Alilaani mashambulizi hayo na kuvitaka vikosi vya ulinzi kuchukua hatua haraka.

"Tumeungana katika kutafuta haki na amani ya kudumu, " Chollom alisema.

Mashambulizi yaliyoanza eneo la Bokkos yalienea hadi eneo jirani la Barkin Ladi ambapo watu 30 walipatikana wamefariki, kulingana na mwenyekiti wa eneo hilo Danjuma Dakil.

Mnamo Jumapili, Gavana wa Jimbo la Plateau Caleb Mutfwang alilaani vurugu hizo, akizitaja kuwa "za kinyama, za kikatili na zisizo na msingi."

Kwa kipindi kirefu, maeneo ya Kaskazini Magharibi na katikati mwa Nigeria yamekuwa yakitishiwa na wanamgambo na majambazi waliojificha kwenye vituo vilivyo ndani ya misitu na kuvamia vijiji ili kupora na kuwateka nyara wakazi kwa ajili ya kudai fidia.

AFP