Tume ya haki za binadamu ya Nigeria ilisema siku ya Ijumaa uchunguzi haujapata "ushahidi" kwamba jeshi la Nigeria liliwashambulia kwa makusudi wanawake na watoto au lilitoa mimba kwa siri katika mapambano yake dhidi ya waasi wa Kiislamu kaskazini mashariki.
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Nigeria, ambayo imeteuliwa na serikali, ilikuwa ikichunguza ripoti tatu za Reuters zilizochapishwa mnamo Desemba 2022 ambazo ziligundua jeshi la Nigeria liliendesha mpango wa siri, wa kimfumo na haramu wa uavyaji mimba na mauaji ya watoto kaskazini mashariki, ambapo uasi umekuwa ukiendelea kwa miaka 15.
Tume hiyo imesema katika ripoti yake kwamba ilifanya uchunguzi wake katika kipindi cha miezi 18 na kuwahoji mashahidi 199, wakiwemo kutoka jeshi, wanamgambo wa zamani, wanawake walioachiliwa kutoka kwa kifungo cha Boko Haram na mashirika ya misaada ya ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya mashahidi waliohojiwa hawakutajwa majina yao.
Miongoni mwa waliohojiwa kwa ajili ya uchunguzi huo ni Mkuu wa Majeshi Chris Musa, ambaye wakati wa ripoti hizo aliongoza kampeni ya kukabiliana na uasi kaskazini-mashariki, mtangulizi wake Jenerali Lucky Irabor na Mkuu wa Majeshi wa zamani Luteni Jenerali Farouk Yahaya.
Jopo la watu saba lililofanya uchunguzi huo lilijumuisha meja jenerali mstaafu, Letam Wiwa, ambaye hapo awali aliwahi kuwa mkuu wa ujasusi wa kijeshi.
Yeye ni kaka mdogo wa Ken Saro-Wiwa, mwanaharakati wa Niger Delta ambaye aliuawa na jeshi mnamo 1995.
"Hakuna ushahidi kuthibitisha kwamba jeshi la Nigeria lilifanya mpango wa siri wa uavyaji mimba kaskazini-mashariki, na kumaliza mimba za maelfu ya wanawake na wasichana walioachiliwa kutoka kwa utumwa wa waasi," ilisema ripoti hiyo, ambayo ilitolewa katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu Abuja.
Jeshi la Nigeria hapo awali lilikanusha matokeo katika ripoti za shirika hilo la habari.
Msemaji wa jeshi Edward Buba hakujibu mara moja ombi la maoni yake mnamo Ijumaa.