Viwanda haramu vya silaha vinazidi kushamiri nchini Nigeria./Picha: Olumuyiwa Adejobi

Vikijificha chini ya mwamvuli wa biashara halali, viwanda hivi haramu vimekuwa tishio kwa usalama wa eneo la Afrika Magharibi.

|Ukubwa wa tishio hili unatokana na polisi kuibua msururu wa viwanda haramu vya bunduki nchini Nigeria.

Silaha za kila aina, kuanzia mifano ya AK-47, bunduki za pipa hadi bastola, zote hizo hutengenezwa na viwanda hivyo.

Oktoba mwaka jana, polisi walivamia moja ya viwanda haramu huko Lagos.

"Angalia namna walivyoitengeneza hii AK-47, ni jambo la kushangaza kwa kweli," alisema msemaji wa Jeshi la Polisi la Nigeria Olumuyiwa Adejobi kupitia ukurasa wa X hivi majuzi, akionesha silaha inayodaiwa kukamatwa kutoka kwa kiwanda haramu cha kutengeneza bunduki katika jimbo la Plateau.

Hivi karibuni, jeshi la Nigeria lilivamia kiwanda kama hicho kwenye Jimbo la Kusini la Delta.

Mtindo huo unaonekana kufahamika, kutoka jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria hadi Lagos kusini magharibi. Maafisa wa usalama huvamia viwanda, kukamata silaha kwa wingi na kukamata watu, ili tu misururu ya risasi iendelee kukua zaidi.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria , Olumuyiwa Adejobi akionesha silaha aina ya AK47 iliyotengenezwa na viwanda hivyo:Picha: /X/OlumuyiwaAdejobi

"Utengenezaji wa silaha haramu umetawala katika sehemu za kusini mashariki na kaskazini kati mwa Nigeria," Sadiq Garba Shehu anaimbia TRT Afrika.

Tatizo la Afrika Magharibi

Tatizo hili sio la Nigeria peke yake. Nchi nyingi, haswa zile zinazopambana na migogoro ya ndani zina makundi sugu kwenye viwanda hivyo.

Kulingana na makala iliyochapishwa kwenye mtandao wa Relief, watengenezaji wa silaha haramu wamekuwepo katika nchi kama Mali, Senegal, Togo, Sierra Leone, Liberia, Guinea, Mali, Benin, Burkina Faso na Ivory Coast kwa muda mrefu.

Ripoti ya 2018 kuhusu ujumuishaji wa jinsia katika amani na usalama ndani ya ECOWAS inasema viwanda hivi vilihusika sana na "umiliki na usambazaji mkubwa wa silaha mikononi mwa raia".

Kando na usambazaji wa silaha ndogo ndogo, mwelekeo huu umehusishwa na kuongezeka kwa migogoro ya ndani katika nchi zote zilizoathirika, hususani Afrika Magharibi.

Mara kwa mara, ECOWAS imezitaka nchi wanachama kuchukua hatua kali na za pamoja ili kuzuia kuenea kwa silaha haramu katika ukanda hiyo.

Viwanda hivi vimeongeza umiliki wa silaha kwa raia./Picha: Reuters

Ingawa serikali nyingi zimepambana na mashambulizi ya silaha, bado viwanda hivi havijadhibitiwa huku zikiendelea kustawi mbele ya macho ya taasisi za usalama.

Mambo ni yale yale

Viwanda haramu vya kutengeneza bunduki nchini Nigeria vinajulikana kwa kutengeneza silaha nyingi.

"Zote hizi hutengenezwa kienyeji kwenye viwanda huko Jos. Vijana hao wana vipaji sana," anasema msemaji wa polisi Adejobi, akiweka picha ya bastola tisa zilizokamatwa kwenye ukurasa wake wa X.

Ni nini kinachopelekea uzalishwaji wa silaha haramu katika ukanda huo?

"Matendo ya kihalifu yanaongeza mahitaji ya silaha za namna hii," anaelezea Kepteni Shehu. "Migogoro ya kikabila na kidini imeanzisha vikundi vya aina hii ambavyo visingeweza kupata silaha kwa njia za halali."

Kulingana na wachambuzi, silaha zinazotengenezwa katika viwanda hivyo haramu zinajumuisha sehemu kubwa ya zile zinazosambazwa. Shehu anasema viwanda vya aina hii huchangia asilimia 40 ya tatizo."

Mabadiliko katika mkakati

Maoni katika mtandao wa kijamii wa Adejobi yanaonesha kwamba Wanigeria wengi wanaamini kwamba vyombo vya usalama vinapaswa kushughulikia tatizo hilo kwa njia tofauti.

Viwanda haramu vya kutengeneza bunduki nchini Nigeria vinajulikana kwa kutengeneza silaha nyingi./Picha: Reuters

"Tunahitaji kuzifanyia kazi, kwa manufaa yetu," msemaji huyo wa polisi aliandika, akitoa maoni yanayopendekeza kwamba mamlaka zinahitaji kutumia "talanta" za wale wanaotengeneza silaha kinyume cha sheria kwa manufaa ya nchi.

"Ni vigumu sana kuwaondoa katika utengenezaji wa bunduki haramu kwani wanasukumwa na pesa na hisia za kidini," anasema Shehu.

TRT Afrika