Kundi la wanamgambo wa  Al-Shabaab limekuwa likishinikiza kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni kutoka Somalia / Picha: AFP

Polisi wa Kenya wamewaua watu 20 wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab kaskazini-mashariki ya Mandera, karibu na mpaka na Somalia.

Washukiwa hao walikuwa wameshambulia gari la maafisa wa polisi wa doria, na kusababisha vita ya risasi, na vifo vya washukiwa 20 na wana usalama wanane kujeruhiwa.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Ogorwen, takriban kilomita 1,050 kutoka jiji kuu la Nairobi.

"Polisi walipata silaha za aina mbalimbali kutoka eneo la uhalifu," Polisi ya Kenya ilisema katika taarifa siku ya Alhamisi.

Uasi wa Al-Shabaab unaendelea kuwa changamoto kwa serikali za Kenya na Somalia.

Kufunguliwa kwa mpaka kumeahirishwa

Siku ya Jumatano, Kenya ilitangaza kuwa imesitisha mipango yake ya kufungua tena mipaka yake na Somalia ambayo ilikuwa imesema itafanya hatua kwa hatua.

Serikali imesema Al-Shabaab tena ni tishio kwa usalama wa taifa.

Kundi hilo la wanamgambo limekuwa likishinikiza kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni kutoka Somalia huku likijaribu kuchukua udhibiti wa operesheni nchini humo.

Jitihada zao, hata hivyo, hazikufaulu.

Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimeshiriki katika operesheni tofauti za kulinda amani nchini Somalia ili kuleta utulivu wa taifa hilo.

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimeanza mchakato wa kusitisha operesheni zake nchini Somalia na kuanza kukabidhi jukumu la usalama kwa serikali ya Somalia.

TRT Afrika