Waziri wa Mambo ya Nje Abderaman Koulamallah amesema  watu 19 waliuawa katika mapigano hayo / Picha: AFP

Watu wenye silaha walijaribu kuvamia majengo ya Rais katika mji mkuu wa Chad N'Djamena siku ya Jumatano, na kupelekea mapigano yaliyosababisha washambuliaji 18 na mwana usalama mmoja kuuawa, serikali ilisema.

Waandishi wa habari wa AFP walisikia milio ya risasi ikiripuka karibu na eneo hilo na kuona vifaru mitaani, huku vyanzo vya usalama vikiripoti kuwa watu wenye silaha walijaribu kuvuka eneo hilo.

Baadae serikali ilisema watu 19 waliuawa katika mapigano hayo, ambapo 18 walikuwa wanachama wa kikosi cha makomandoo cha askari 24 walioanzisha mashambulizi hayo.

"Kulikuwa na watu 18 waliokufa na sita kujeruhiwa" kati ya washambuliaji "na tulipata kifo kimoja na watatu kujeruhiwa, mmoja wao vibaya," msemaji wa serikali na Waziri wa Mambo ya Nje Abderaman Koulamallah aliiambia AFP.

Saa chache baada ya milio ya risasi kusikika, Koulamallah alionekana kwenye video iliyotumwa kwenye mtandao wa Facebook, akiwa amezungukwa na wanajeshi akisema "hali imedhibitiwa kabisa ... jaribio la shambulizi lilisitishwa."

Chanzo cha usalama kimesema washambuliaji hao ni wanachama wa kundi la wanamgambo wa Boko Haram, ambalo vikosi vya Chad vinapigana navyo katika eneo la magharibi la Ziwa Chad ambalo linapakana na Cameroon, Nigeria na Niger.

Chad ambayo haina bandari inakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram.

Hivi majuzi ilihitimisha makubaliano ya kijeshi na ukoloni wa zamani Ufaransa na imekuwa ikishutumiwa kwa kuingilia mzozo unaoikumba nchi jirani ya Sudan.

barabara kufungwa

Vyanzo kadhaa vya usalama vilisema kuwa kikosi cha makomando wenye silaha kilifyatua risasi ndani ya ofisi ya rais mnamo Jumatano jioni karibu 7:45 pm (1845 GMT), kabla ya kuzidiwa nguvu na walinzi wa rais.

Barabara zote zinazoelekea kwenye ofisi ya Rais zilifungwa na mizinga kuonekana mitaani, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP katika eneo la tukio.

Wakati raia wakikimbia kutoka katikati mwa jiji kwa magari na pikipiki, polisi wenye silaha walionekana katika maeneo kadhaa katika wilaya hiyo.

Saa chache kabla ya mapigano kuanza, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alikutana na Rais Mahamat Idriss Deby Itno na maafisa wengine wakuu.

Utawala wa Chad

Jenerali Déby alitawazwa kama kiongozi wa Chad na jeshi baada ya baba yake, Idriss Déby Itno, kuuawa wakati wa vita na vikosi vya waasi mnamo Aprili 2021

Mei 2024 Chad ilifanya uchaguzi mkuu na Deby alitangazwa mshindi na hivyo kuhalalisha mamlaka yake.

Chad, koloni la zamani la Ufaransa lilikuwa mwenyeji wa kambi za mwisho za kijeshi za Ufaransa katika eneo hilo linalojulikana kama Sahel, lakini mwishoni mwa Novemba 2024, Chad ilimaliza makubaliano ya ulinzi na usalama na Paris, na kuyaita "ya kizamani".

Takriban wanajeshi elfu moja wa Ufaransa nchini humo wako katika harakati za kuondolewa.

TRT Afrika