Tume ya maendeleo Rwanda, yaani Rwanda Development Board, imetenga Septemba Mosi kama siku ya kuwapa majina watoto wa sokwe 23.
Sherehe ya kuwapa sokwe majina nchini humo inaitwa Kwita Izina, Ilianza mwaka 2005 na hadi sasa watoto 374 wa sokwe wamepewa majina.
"Majina ya wale watu watakaochaguliwa kuwapa sokwe majina mwaka huu yatafichuliwa siku ikikaribia. Wanajumuisha washirika mashuhuri, wahifadhi, watu wa kimataifa na wa ndani, pamoja na watu mashuhuri na marafiki wa Rwanda," taarifa ya Rwanda Development Board imesema.
Sherehe hiyo itafanyika katika sehemu ya hifadhi ya kitaifa ya Volcano huko Kinigi, Wilaya ya Musanze.
Mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Claire Akamanzi amesema katika taarifa kuwa,
"Takwimu za sasa za utalii zinaonyesha kuwa Rwanda ilizalisha dola za Marekani milioni 247 katika nusu ya kwanza ya 2023, ongezeko la asili mia 56 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 158 katika kipindi kama hicho mwaka 2022."
Sokwe katika misitu ya Rwanda ni kivutio kikubwa cha utalii nchini humo.
Takwimu zaonesha kuwa mwaka 2022 utalii wa sokwe ulifanya vizuri zaidi katika sekta ya utalii , na serikali inatazamia kuwa hali hiyo pia itaongezeka katika mwaka wa 2023.
Sherehe ya Kwita Izina ni nini?
Kulingana na maelezo ya Rwanda Development Board sherehe ya kuwapa majina sokwe inayoitwa Kwita Izina imetokana na utamaduni wa karne nyingi ambapo Wanyarwanda huwapa majina watoto wao mbele ya familia na marafiki.
Kwa miongo mitatu kabla ya sherehe ya kwanza rasmi ya kuwapa sokwe majina, walinzi wa mbuga na watafiti walitaja watoto wa sokwe kwa ajili ya kufuatilia kila sokwe katika familia na makazi yao.
Mnamo mwaka 2005, Rwanda ilianza kuwapa majina sokwe katika kile ambacho kimekuwa sherehe ya ulimwengu ya asili.
Rwanda Development Board inasema kwa kuwapa majina wanyama hawa wakubwa, inawapa thamani wanayostahili.
Serikali inasema sherehe hii ni fursa ya kuwashukuru wanajamii wanaoishi karibu na makazi ya sokwe, Hifadhi ya Kitaifa ya Volcano, washirika wa utafiti, madaktari wa mifugo na wahifadhi waliojitolea, walinzi na wafuatiliaji wanaolinda sokwe kila siku.