Wanasheria barani Afrika wamepeleka shauri lao mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) wakiitaka taasisi hiyo kuitangaza hukumu hiyo kama ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu.
Chini ya mwamvuli wao wa PALU, wanasheria hao wanasisitiza kuwa hukumu hiyo ni kinyume na Mkataba wa Haki za Binadamu barani Afrika.
“Nchi nyingi za Afrika zimeachana na hukumu hii. Ni wakati muafaka kutambua kuwa hukumu ya kifo si ubinadamu na ni ukiukwaji wa haki ya kuishi,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa PALU, Donald Deya.
Katika ombi lake kwa AfCHPR, PALU imeanisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nchi za Afrika zimeondoa hukumu hiyo huku nyingine zikiwa hazitekelezi sheria hiyo.
Ni nchi mbili tu barani Afrika ambazo zilitekeleza sheria hiyo mwaka 2023.
Nchi hizo ni Misri na Somalia.
Katika ombi lake kwa Mahakama ya Afrika, PALU inasema kuwa adhabu ya kifo inakabiliwa na kasoro za kiutaratibu huku ikitolewa kwa njia za kibaguzi kwa kuzingatia jinsia, umri, ulemavu wa akili, umaskini, vikwazo vya lugha na misimamo ya kisiasa, kinyume na kufungu na 4 cha Kifungu cha 4 cha Mkataba wa Haki za Binadamu barani Afrika.
“Kupitia ombi hilo, tunaiomba Mahakama ya Afrika itoe maoni yake kuhusu adhabu ya kifo, ikiwa ni pamoja uasili wa ukatili wa adhabu hiyo pamoja na vyombo husika vya haki za binadamu na kutoa mwongozo wake kwa nchi wanachama”, Deya alisema.