Wanajeshi wa nchi hizo mbili wamekutana ndani ya msitu mkubwa wa Kongo. Picha: KDF

Wanajeshi wa nchi hizo mbili wamekutana ndani ya msitu mkubwa wa Kongo, huku wanajeshi wa Kenya kutoka kikosi maalum cha QRF, wanaojulikana kwa utaalam wao katika vita vya msituni, wakiungana na wenzao kutoka Brazil, walio na maarifa ya kina ya mazingira ya kitropiki na uhodari wa mbinu za kupambana na waasi.

Wanajeshi hao wanatarajiwa kupitia mafunzo ya ukakamavu wa mwili na kiakili. Mafunzo hayo madhumumi yake ni kuwaandaa kwa hali isiyotabirika ya vita vya msituni kwa kuwapa ujuzi wa kuishi, mbinu za doria na huduma ya matibabu katika hali ngumu.

Ushirikiano wa wanajeshi hao unakusudia kuleta pamoja nguvu za vitengo vyote viwili na kukuza ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazosubiri misheni ya kulinda amani katika mazingira yenye ukosefu usalama na uhasama.

Mafunzo hayo maalum yametokana na ushirikiano wa msingi kati ya walinzi wa Kenya chini ya kitengo cha 'Quick Reaction Force (QRF)' na kikosi cha Brazil cha 'Jungle Warfare Mobile Training Team (JWMTT).

"Vita vya msituni vina changamoto za kipekee zinazohitaji ujuzi na mbinu maalum. Kwa kuunganisha uzoefu wetu na kujifunza zaidi kutoka wenzetu kutoka Brazil, tunatumai kuwa na ufanisi zaidi katika dhamira yetu ya kulinda raia na kudumisha amani katika eneo hili,” amesema Luteni Kanali Ambrose Mwabi, Afisa Mkuu wa kikosi cha QRF cha Kenya.

Juhudi hii ya mafunzo ya pamoja inaonekana kama hatua muhimu katika juhudi za kimataifa za kulinda amani, kudhihirisha kujitolea kwa mataifa haya mawili ili kuongeza uwezo wao na kuchangia utulivu wa eneo hilo.

"Utofauti wa askari wetu na utaalamu tulionao kutokana na kufanya operesheni ndani ya msitu Amazon, unatufanya kuwa mshirika muhimu katika mafunzo haya. Kupitia ushirikiano na wenzetu wa Kenya, tunakusudia kuongeza kiwango cha vikosi vya kulinda amani katika mazingira ya msituni,” Luteni Kanali wa Brazil Joao Carlos Duque, anayeongoza Kitengo Cha Brazil alisema.

Kulingana na taarifa ya wanajeshi wa KDF, jitihada za nchi hizo mbili kukabilina na ugumu wa vita vya msituni inathibitisha kujitolea kwao kulinda amani dhaifu wa Mashariki ya DRC na kuwa mwangaza wa matumaini kwa wakaazi wa mkoa huo.

TRT Afrika