Mkuu wa majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Francis Ogolla amewatembelea vikosi vya Kenya chini ya kikosi cha Kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuondoka rasmi kwa vikosi hivyo.
Wanajeshi wa Kenya ni miongoni mwa vikosi vya ulinzi waliokuwa chini ya EACRF na MONUSCO.
Jenerali Francis Ogolla alizuru makao makuu ya vikosi vya EACRF na kuzungumza na vikosi vya Kenya vilivyoko Goma, kambi ya Kibumba, na Kibati ndani ya Eneo la Nyiragongo, Kivu Kaskazini.
Haya yanajiri kufuatia kupelekwa kwa wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) na kutorefushwa kwa muda wa kuwepo kwa EACRF. Vikosi hivyo vinatakiwa kuondoka kabla ya tarehe 8 Desemba 2023.
Ogolla alikaribishwa katika makao makuu ya EACRF, na Kamanda wa Kikosi cha EACRF Meja Jenerali Aphaxard Kiugu, akiandamana na Naibu Makamanda wa Kikosi Brigedia Jenerali Emmanuel Kaputa wa (DRC), Brigedia Jenerali Gregoire Ndorarigonya (Burundi), Mkuu wa Wafanyakazi Brigedia Jenerali Michael Kibuye (Uganda), Mkuu Wa Operesheni Kanali Jok Akech (Sudan Kusini), na Maafisa wengine muhimu wa ngazi za juu.
Ziara ya Ogolla inakuja wakati ambapo hali ya usalama Mashariki mwa DRC haijulikani kufuatia uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hapo awali, vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na M23 viliingia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yakitumika hadi yalipovunjwa mnamo Oktoba 2023.
Tangu kupelekwa kwake, kikosi cha EACRF kilifanikiwa kuzuia tishio la karibu kwa mji wa Goma, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma, na kuwezesha uondoaji wa M23 kutoka maeneo karibu na Goma kando ya barabara ya Natia Namba 2 na Barabara ya Mkoa namba 1030.
"Ni lazima nishukuru serikali ya DRC kwa kuwa mwenyeji mwema na kwa kutoa msaada unaohitajika kwa walinzi wa EACRF licha ya changamoto za asili," Ogolla alisema.
Ogolla pia aliendelea kusisitiza kujitolea kwa Kenya kuendelea kushiriki katika mipango ya amani ya kikanda hadi utulivu kamili utakapopatikana mashariki mwa DRC na kudumu kwa amani na usalama.