Wanajeshi wa Burundi chini ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wameanza kuondoka katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Kuondolewa kwa wanajeshi 2,000 kulianza Jumanne, wakati tume ya kulinda amani ilipokabidhi kambi ya operesheni katika Jimbo la Hirshabelle kwa jeshi la Somalia, ATMIS ilisema katika taarifa.
Luteni Kanali Richard Binyenimana, Kamanda wa Kituo cha Uendeshaji cha Cadale (FOB), alisema wanajeshi wote wa Burundi watakuwa wameondoka Somalia mwishoni mwa Juni.
Kamanda wa Jeshi la Kitaifa la Somalia Meja Bashir Ahmed sasa atakuwa msimamizi wa kituo cha uendeshaji huko Hirshabelle katika juhudiu za ATMIS "kurejesha udhibiti kwa shirikisho la Somalia".
Kujitolea kwa wanajeshi
Ijumaa iliyopita, wajumbe wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa Umoja wa Afrika, (AU) walikagua kituo cha uendeshaji cha Cadale kabla ya kufanyika shughuli ya kukabidhi
Ujumbe huo uliongozwa na mwakilishi maalum wa AU nchini Somalia na Mkuu wa ATMIS, Balozi Mohamed El-Amine Souef, na Mkuu wa ofisi ya msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOS), Aisa Kirabo Kacyira.
Kacyira aliwapongeza wanajeshi wa Burundi kwa mchango wao katika kuleta utulivu wa Somalia.
"Mnaondoka kwa heshima na hali ya kufanikiwa. Tunataka kuwashukuru kwa kufanya kazi ngumu ya kujitolea. Ninafahamu kuwa askari walipoteza maisha na tunawaheshimu leo," alisema wakati akiwahutubia wanajeshi hao Ijumaa.
Kituo cha uendeshaji cha Cadale kiko kando ya mwambao wa Somalia, kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.
Kuondoka DRC
Kuondolewa kwa wanajeshi wa Burundi kutoka Somalia kunakuja siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa umeanzisha utaratibu wa kuondoa ujumbe wake wa kulinda amani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, (DRC).
Mkuu wa timu ya walinda amani, Bintou Keita, alisema kuondolewa kwa vikosi hivyo kunakuja baada ya "kutimizwa kwa masharti muhimu ya mpango wa mpito".