wanafunzi kutoka Sudan Picha: Muhimbili Twitter

Wanafunzi takriban 150 wa tiba kutoka Sudan ambao wameathiriwa na vita wamehamishiwa Tanzania ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo, kulingana na ripoti za ndani.

Wanafunzi hao kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi, na Teknolojia (UMST) huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, walipokelewa Jumatatu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Wanafunzi hao wako katika mwaka wa tano wa masomo ambao unahitaji mafunzo ya vitendo, Mkurugenzi wa hospitali Mohamed Janabi alisema kwa mujibu wa ripoti.

Madaktari wataalamu watashiriki kusimamia mafunzo yao katika idara mbalimbali za hospitali, aliongeza.

Utulivu uliripotiwa katika sehemu kubwa za Sudan Jumatatu baada ya pande zinazohasimiana kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano ya masaa 72 Jumapili. Makubaliano hayo yalisimamiwa na Saudi Arabia na Marekani na yanakusudia kupunguza mvutano na kuruhusu harakati na utoaji wa misaada ya kibinadamu.

"Hospitali ya Muhimbili itawasaidia katika masomo yao, kama wanavyofanya na wanafunzi wa ndani, na baada ya kukamilisha masomo yao, wanaweza kupewa fursa ya kufanya mafunzo ya vitendo (internship) katika hospitali," alisema.

Hospitali nyingi nchini Sudan zilizoko karibu na maeneo ya mapigano zimefungwa, kulingana na madaktari wa ndani.

Chama cha Madaktari Sudan kimesema hospitali 59 kati ya 82 huko Khartoum na majimbo mengine zimezimwa.

Zaidi ya watu 800, wakiwemo watoto 330, wameuawa katika mzozo huo, na angalau wengine milioni 2.2 wamepoteza makazi yao, na nusu ya wakimbizi hao ni watoto, kulingana na Umoja wa Mataifa.

TRT Afrika na mashirika ya habari